Maelfu ya wafuasi wa chama cha Muslim Britherhood wameandamana kwenye miji mbalimbali nchini humo mara baada ya sala ya Ijumaa wakishinikiza kurejeshwa madarakani kwa kiongozi wao, Mohamed Morsi. Maandamano haya ya mara baada ya sala ya Ijumaa yanafanyika wakati ambapo jeshi limeonya dhidi ya kufanyika kwa maandamano ya vurugu na kwamba halitavumilia kuona maandamano hayo yakigeuka kuwa vurugu. Wafuasi hao wa Muslim Brotherhood wameendelea kupuuza tangazo la rais wa mpito, Adly Mansour ambaye amewataka wafuasi hao kuwa watulivu na kuapa kuilinda nchi yake dhidi ya watu wachache wanaotaka kuharibu amani ya nchi.
Maandamano makubwa yameshuhudiwa kwenye eneo la Rabaa al-Adawiya mjini Cairo ambako wafuasi wa Morsi wamepiga kambi toka kiongozi wao alipoondolewa madarakani tarehe 3 ya mwezi July mwaka huu. Viongozi wa Muslim Brotherhood wameyaita maandamano ya hii leo kama ni ya kuvunja mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo na kumrejesha madarakani rais wao Mohamed Morsi. Maandamano haya yanafanyika ikiwa ujumbe wa Umoja wa Ulaya EU uliokuwa nchini humo ukikiri kuwa mzozo huo bado mgumu kuutatua kutokana na pande hizo mbili kutokuwa tayari.
Hapo jana msemaji wa Muslim Brotherhood, Gehad el-Haddad alisema kuwa baada ya kukutana na ujumbe wa EU walitoa mapendekezo yao ya namna ya kusaka suluhu ya kisiasa nchini Misri. Viongozi hao wakaweka wazi nia yao ya kushiriki mazungumzo licha ya kuendelea na msimamo wao wa kutaka Mohamed Morsi arejeshwe madarakani.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO