Friday, July 26, 2013

MGOMO WAFANYIKA TUNISIA KUPINGA KIFO CHA MBUNGE WA UPINZANI

Mgomo wa Kitaifa umeitishwa nchini Tunisia ukiwa na lengo la kuonesha kukasirishwa na hatua kuuawa kwa Mbunge wa Upinzani nchini humo Mohamed Brahmi ambaye anatajwa alikuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Chama Cha Ennahda. Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini Tunisia UGTT limeitisha mgomo wa kitaifa utakaoambatana na m,aandamano kuonesha kuchukizwa kwao na mauaji ya Mbunge Brahim. Brahmi alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake na watu waliokuwa wamejihami na silaha na hadi sasa hawajulikani kina nani na hakuna Kundi lolote ambalo limejitangaza kutekeleza mauaji hayo. Maandamano makubwa yalishuhudiwa usiku wa alhamisi kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji la Tunis kushinikiza Jumuiya ya Kimataifa kulaani kile ambacho kimefanywa huku wengi wakinyoosha kidole cha lawama kwa Serikali.
Shirika la Ndege nchini humo la Tunisair limetangaza kufuta safari zake zote za ndege kitu ambacho kinatajwa kitaathiri shughuli nyingi ikiwa ni sehemu ya kuonesha kupinga kwao mauaji hao ya Brahmi. Chama Tawala cha Ennahda kimejitenga na mauaji hayo ya Mbunge Brahmi na kusema madai ambayo yanatolewa na familia kuwalenga wao kupanga na kutekeleza tukio hilo hayana ukweli wowote. Jeshi la Polisi limekuwa kwenye kibarua kizito cha kupambana na waandamanaji waliojitokeza kwenye mitaa ya Tunis na Sidi Bouzid eneo ambalo linatajwa kuwa chanzo cha mapinduzi yaliyomuangusha Rais Zine El Abidine Ben Ali. Brahmi mtu ambaye alikuwa na mrengo wa kushoto anakumbukwa vyema kwa kuanzisha maandamano makubwa ya kitaifa ya saa mbili yaliyosababisha kuangushwa kwa Utawala wa Ben Ali.
Dada wa Marehemu Chhiba Brahmi amekituhumu waziwazi Chama Tawala cha Ennahda kuhusika na mauaji ya ndugu yao na wametaka uchunguzi huru ufanyike kubaini waliohusika kwenye tukio hilo. Mkuu wa Chama Cha Ennahda Rached Ghannouchi amekanusha kwa nguvu zake zote madai ya kwamba wao ndiyo wamehusika kwenye mauaji ya Brahim na kusisitiza mauaji hayo ni janga kwa Tunisia. Mohamed Brahim anakuwa mwanasiasa wa pili kuuawa nchini Tunisia baada ya mwezi februari kutekelezwa mauaji ya mwanasiasa mwingine wa upinzani Chokri Belaid aliyeuawa nje ya nyumba yake.
Marekani imelaani mauaji hayo huku Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton akitoa tamko hilo hilo wakati Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binadamu Navi Pillay akitaka uchunguzi wa haraka ufanyike.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO