Sunday, July 07, 2013

UTATA WAGUBIKA JUU YA CHEO CHAEL BARADEI

Uteuzi wa Mohammad El Baradei kama Waziri Mkuu wa Muda Misri umegonga mwamba baada ya chama cha pili kwa ukubwa cha Kiislamu,  An Nour, kupinga uteuzi wa mwanasiasa huyo mashuhuri mwenye mitazamo ya kiliberali.
Chama cha An Nour kinaunga mkono ramani ya njia iliyotayarishwa na jeshi kwa lengo la kuandaa uchaguzi mkuu nchini Misri. Naibu Mwenyekiti wa An Nour Said Ahmad Khalil amesema chama chake kitajiondoa katika mkondo wa mpito wa kisiasa iwapo jeshi litasisitiza kumteua El Baradei. Kufuatia upinzani huo rais wa muda wa Misri Adli Mansour jana usiku alibatilisha uamuzi wake wa awali wa kumtangaza El Baradei kuwa waziri mkuu.
Huku hayo yakijiri hali bado si shwari nchini Misri na machafuko yameripotiwa kuendelea baina ya wafuasi na wapinzani wa Mohammad Mursi aliyekuwa rais hadi alipoondolewa madarakani na jeshi Julai Tatu.
Wakati huo huo Harakati ya Ikwanul Muslimin imesema nchi za Magharibi ziliunga mkono mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Mursi. Mohammad El Betlagi kiongozi mwandamizi wa Ikwan amesema uungaji mkono huo utapelekea kuongezeka chuki dhidi ya Marekani na nchi za Ulaya.
Zaidi ya watu 36 walipoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa Ijumaa kufuatia machafuko yaliyoibuka baina ya makundi hasimu baada ya Rais Mohammad Mursi kutimuliwa madarakani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO