Jumuiya kubwa zaidi ya Kiislamu nchini Uingereza, imetaka kuchukuliwa hatua na mikakati ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Katika barua kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, Faruq Murad Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini humo, ameashiria ongezeko la mashambulizi dhidi ya Waislamu na kuitaka serikali na vikosi vya polisi nchini humo kuchukua hatua ya pamoja katika kuzuia hujuma hizo dhidi ya Waislamu. Baada ya kuuawa askari mmoja wa nchi hiyo na watu wawili mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, makundi yenye kufurutu mipaka ya mrengo wa kulia, yalitumia vibaya mauaji hayo kushadidisha vitendo vya kikatili dhidi ya Waislamu. Tokea wakati huo, misikiti na makaburi ya Waislamu hayajasalimika na mashambulizi ya makundi hayo wenye misimamo ya kufurutu mipaka. Vitendo vya ubaguzi dhidi ya Uislamu na kukanyagwa haki za Waislamu, vimeshtadi sana nchini humo. Aidha ongezeko la propaganda chafu za vyombo vya habari vya Uingereza, linatajwa kuwa sababu ya kushtadi ubaguzi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Vitendo vya kufurutu mipaka vinavyofanywa na magenge ya magaidi, vimekuwa chanzo na sababu ya makundi ya mrengo wa kulia yenye kufurutu mipaka na serikali ya London, kushadidisha mashinikizo na sheria kali dhidi ya Waislamu. Hata hivyo propaganda hizo na hatua za kibaguzi dhidi ya Uislamu, zimekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa makundi yanayopinga ubaguzi wa rangi, vita na ya kutetea haki za binaadamu nchini Uingereza. Pamoja na taasisi na jumuiya za Kiislamu kulaani vikali mauaji ya mwezi Mei dhidi ya askari wa nchi hiyo, lakini bado propaganda dhidi ya Uislamu zingali zinaendelea katika baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo ya Ulaya. Aidha ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla umeongezeka katika fikra za waliowengi, licha ya viongozi wa Uingereza akiwemo David Cameron Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kutoa azimio lililo wazi la kuwataka wananchi kudumisha umoja na kusisitiza kutohusika Waislamu katika mauaji ya askari huyo. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, serikali ya London na vyombo vya habari vya nchi hiyo, vimekuwa vikiendesha kampeni za kibaguzi kwa muda mrefu dhidi ya Uislamu hususan baada ya tukio la Septemba 11 nchini Marekani. Ni kwa ajili hiyo, ndio maana muungano wa Kiislamu nchini humo, ukaitaka serikali hiyo, kuzuia mashambulzi dhidi ya Waislamu na vituo vyao vya ibada, mashambulizi ambayo kwa hakika yanafanyika kwa baraka za serikali na polisi ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO