Ismail Hania, Waziri Mkuu wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina amewaomba viongozi wa serikali ya Misri wakifungue tena kivuko cha Rafah kilichoko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Ukanda wa Gaza wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Hania alitoa wito huo katika hotuba za Sala ya Idil Fitri iliyosaliwa jana huko Gaza na kuwataka viongozi wa Misri wakifungue tena kivuko hicho kwa ajili ya Wapalestina ili wananchi hao madhulumu waweze kuingia na kutoka kirahisi na pia kuwepesisha uingizaji wa bidhaa zinazohitajika huko Gaza. Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali halali ya Palestina yenye makao yake huko Ukanda wa Gaza ilitahadharisha juu ya kutokea maafa ya kibinadamu katika eneo hilo kutokana na mzingiro uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwaka 2007. Naye Muhammad al Katri, afisa mwanadamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Wapalestina wa Gaza hususan wagonjwa wanashindwa kufuatilia matibabu yao nje ya Palestina kutokana na kufungwa mara kwa mara kivuko cha Rafah na kwamba wagonjwa wanaohitaji kupelekwa ng'ambo kwa matibabu wanakabiliwa na hatari ya kifo. Ameongeza kuwa vizuizi katika kivuko cha Rafah vimeshadidishwa na serikali ya Misri tangu rais wa nchi hiyo Muhammad Morsi alipong'olewa madarakani.
Wakati huohuo jumuiya na taasisi za masuala ya sheria huko Ukanda wa Gaza zimetoa taarifa zikitahadharisha kwamba kufungwa kivuko cha Rafah katika mpaka wa pamoja wa Misri na Ukanda wa Gaza kumesababisha matatizo mengi kwa eneo hilo. Jumuiya hizo zimesema kuendelea mzingiro dhidi ya Gaza na kufungwa vivuko vya kuingilia na kutokea katika eneo hilo kunakiuka sheria za kimataifa, na zimezitaka jumuiya za kimataifa zifanye juhudi kuhakikisha mzingiro uliowekwa dhidi ya Gaza unaondolewa. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kwa upande wake imeikosoa serikali ya Misri kutokana na vizuizi vikali inavyowawekea Wapalestina. Katika ripoti yake, OIC imesema matukio ya hivi karibuni nchini Misri yamekuwa na taathira mbaya mno kwa maisha ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza na kuwataka viongozi wa Cairo wachukue hatua za lazima kuhusiana na kivuko cha mpakani cha Rafah ili kupunguza mateso na machungu wanayopata Wapalestina.
Kwa sasa kuna wasafiri wapatao 250 wanaopita kwenye kivuko cha Rafah kwa siku ambapo kabla ya matukio ya hivi karibuni nchini Misri, idadi hiyo ilikuwa ikifikia watu elfu moja. Hadi sasa zaidi ya Waplestina 460 wameshafariki dunia kutokana na uhaba wa dawa na vifaa vya tiba uliosababishwa na mzingiro wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza, na hivi sasa maisha ya mamia ya wagonjwa wengine wa Kipalestina yako hatarini kutokana na hali hiyo. Kutokana na kuvurugika hali ya mambo nchini Misri baada ya kung'olewa madarakani rais wa nchi hiyo Muhammad Morsi, kivuko cha Rafah ambayo ndiyo njia pekee ya kuingilia na kutokea Wapalestina wa Gaza imefungwa rasmi na huwa inafunguliwa kwa muda tu katika siku makhsusi
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO