Wednesday, August 07, 2013

UWANJA WA NDEGE WA KENNYATTA WAWAKA MOTO

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta katika mji mkuu wa Kenya Nairobi umeharibiwa kufuatia moto uliozuka alfajiri ya leo. Taarifa za awali zinasema kuwa, moto uliozuka leo katika uwanja huo umeharibu vibaya sehemu kubwa ya sehemu ya kufikia abiria uwanjani hapo. Kufuatia tukio hilo, serikali ya Kenya imetangaza kufuta kwa muda safari zote za ndege za ndani na za kimataifa na kuzuia kutua uwanjani hapo ndege, hata kwa dharura. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya David Kimaiyo amesema kuwa, hakuna majeruhi yeyote aliyeripotiwa kufuatia ajali hiyo ya moto. Taarifa za awali zinasema kuwa, moto huo ulianzia katika kitengo cha uhamiaji sehemu wanapogongewa muhuri abiria katika pasi zao za kusafiria kwa ajili ya kuingia ndani na kisha baadaye kusambaa katika sehemu ya abiria ya kuchukulia mabegi. Taarifa zaidi zinasema, moto huo ulianza saa kumi na moja alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki na kuendelea kwa muda wa masaa matatu. Shirika la Ndege la Kenya, "Kenya Airways" limetuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter likiwataka abiria wake kutoelekea katika uwanja wa ndege. Rais Uhuru Kenyatta ametembelea eneo la tukio hilo majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki. Tukio hilo linatarajiwa kukwamisha safari nyingi za ndege zinazotumia uwanja huo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO