Thursday, August 15, 2013

W/MKUU WA MISRI ARIDHIA MAUAJI YA WANANCHI

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Misri inayoungwa mkono na jeshi ametetea uamuzi wa serikali kushambulia mikusanyiko ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Muhammad Mursi uliosababisha mauaji makubwa ya raia na kusema kwamba serikali haikuwa na chaguo lingine zaidi ya hilo.
Hazem al Beblawi amesema, uamuzi wa kuvunja kambi za waandamanaji haukuwa rahisi lakini jambo hilo limetekelezwa baada ya serikali kujitahidi kusuluhisha na kushindwa. Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya mpito ya Misri Mohammed Ibrahim amesema kuwa, wafuasi wa Muhammad Mursi rais aliyepinduliwa hawataruhusiwa tena kufanya mkusanyiko wowote katika eneo lolote la nchi hiyo. Ibrahim ametoa matamshi hayo baada ya jeshi la Misri jana kutumia nguvu kuvunja mkusanyiko ya wafuasi hao mjini Cairo ambapo mamia ya watu waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
Wakati hayo yakiripotiwa viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin wametiwa mbaroni na askari usalama wa Misri waliposhambulia mikusanyiko ya maelfu ya wafuasi wa Mursi mjini Cairo. Miongoni mwa viongozi hao waliokamatwa ni Muhamed al Beltagy, Essam al Arian, msemaji wa harakati hiyo Ahmed Aref na kiongozi wa kiitikadi wa Ikhwanul Muslimin Abdul Rahim al Bar.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO