Saturday, April 20, 2013

ISRAEL YATIWA WASIWASI NA MAJESHI YA MISRI


Hatua ya jeshi la Misri ya kutuma vikosi vyake katika eneo la Sinai imewatia wasiwasi maafisa usalama wa utawala wa Kizayuni. Maafisa hao wamesema wametiwa wasiwasi na hatua ya Misri ya kutuma wanajeshi wake katika jangwa la Sinai bila ya kuwasiliana kwanza na utawala huo. Viongozi wa Israel wameeleza kuwa jeshi la Misri mwezi uliopita lilituma kundi la wanajeshi huko Sharm Sheikh bila ya kwanza kuwasiliana na utawala wa Kizayuni kwa shabaha ya kuulinda mfereji wa Suez na kwamba wanajeshi wengi wa Misri wametumwa katika eneo la magharibi mwa jangwa la Sinai.
Wakati huo huo weledi wa mambo wanasema kuwa kuongezwa idadi ya wanajeshi wa Misri huko Sinai si tu kuwa kumevuruga mlingano wa nguvu za kijeshi, bali hatua hiyo ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Misri na Israel.

BALOZI WA MAREKANI NCHINI LEBANON APEWA ONYO

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah ameonya njama za Marekani za kutaka kuuhamisha mgogoro wa Syria na kuutumbukiza nchini Lebanon. Sheikh Naeem Qassim amemuambia Bi. Maura Connelly Balozi wa Marekani mjini Beirut kwamba makundi yote ya kisiasa nchini Lebanon yanaelewa jinsi ya kuendesha mambo ya nchi yao kwa mujibu wa mashirikiano ya pande zote. Amesisitiza kwamba Hizbullah haikubali kuona mgogoro wa Syria unahamishiwa nchini Lebanon. Sheikh Naeem Qassim ameongeza kuwa, Lebanon haihitajii maelekezo ya aina yoyote kutoka kwa Maura Connelly au Marekani kuhusiana na zoezi la uchaguzi nchini humo. Imeelezwa kuwa, Balozi wa Marekani mjini Beirut daima amekuwa akiingilia masuala ya ndani ya Lebanon, ili kuzusha na kushadidisha hitilafu kati ya vyama na makundi ya kisiasa nchini humo.

AZERBAIJAN; HATUKUBALI KUTUMIKA ARDHI YETU KUISHAMBULIA IRAN

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa  Jamhuri ya Azerbaijan amesema kuwa, Baku haitakuwa kituo cha kijeshi cha Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na uwezekano wa kufanyika shambulio la kijeshi  dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Elman Abdullayev ambaye hapo kesho ataongoza ujumbe wa nchi yake huko Tel Aviv ameongeza kuwa, serikali ya Azerbaijan inapinga chokochoko zozote zile dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, nchi hiyo kamwe haitakubali kutoa rufsa kwa Marekani na Israel kutumia ardhi yake  kuishambulia kijeshi Iran.  Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Azerbaijan ametaka kadhia ya nyuklia ya Iran itatuliwe kwa njia za kidiplomasia. Ameongeza kuwa, iwapo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zitaamua kuishambulia Iran, Jamhuri ya Azerbaijan haitaegemea upande wowote kwenye mgogoro huo, na wala haitakubali kutumiwa ardhi yake dhidi ya Iran.

MATATIZO MAKUBWA YAZIDI KUUKUMBA UKANDA WA GHAZA


Kamati ya Wananchi ya Kupambana na Mzingiro katika Ukanda wa Gaza imetangaza kwamba wakazi wa ukanda huo wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa uhaba wa umeme, maji safi ya kunywa na matatizo ya kiafya. Utawala haramu wa Israel umekuwa ukiuzingira ukanda huo tokea angani ardhini na baharini tangu mwaka 2006, jambo ambalo limewasababishia wakazi wake matatizo mengi ya kiuchumi, kiafya na kijamii. Suala hilo limezipelekea taasisi muhimu za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, mashirika ya haki za binadamu, wataalamu na shakhsia mbalimbali wa kieneo na kimataifa kuonya kwamba mgogoro na maafa ya binadamu yanaweza kutokea wakati wowote katika ukanda huo. Tatizo kubwa zaidi kati ya matatizo hayo ni uhaba na kukatwa mara kwa mara umeme na utawala haramu wa Israel, jambo ambalo limewaletea machungu mengi wakaazi wa ukanda huo.
Hatua ya utawala haramu wa Tel Aviv ya kukata umeme mara kwa mara katika misimu ya vipindi baridi imewalazimu wakazi wa Ukanda wa Gaza kutumia mishumaa kuleta joto katika nyumba zao suala ambalo mara nyigi limekuwa na matokeo hatari ya kuteketea kwa nyumba hizo na kuwaua wanaoishi humo. Hivi sasa ambapo kipindi cha joto kinakaribia ukataji huo wa umeme unaweza pia kuwa na matokeo mabaya kwa wakazi wa Ukanda huo. Uhaba wa maji safi pia umekuwa na madhara makubwa kwa wakazi wa Gaza wapatao milioni 1.7. Licha ya hayo maji yanayoruhusiwa kuingia katika Ukanda wa Gaza na utawala haramu wa Israel hayaoani na viwango vya kimataifa vilivyoainishwa na Shirika la Afya Duniani WHO. Asilimia 95 ya maji yanayotumiwa na wananchi wa Gaza ni ya chumvi na asilimia 5 iliyosalia pia imechanganyika na mada za kemikali ambazo humwagwa kwenye maji hayo na utawala wa Israel. Sehemu kubwa ya wananchi hao pia hawana uwezo wa kiuchumi wa kijidhaminia maji hayo ambayo huuzwa kwa bei ghali na wafanyabiashara wa Kizayuni. Sababu kuu ya kuenea magonjwa mbalimbali katika Ukanda wa Gaza ni kiwango cha chini cha maji wanayokunywa na kutumia katika kukidhi mahitaji yao mengine. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Shirika la Afya Duniani likaonya mara kwa mara katika ripoti zake kuhusiana na hatari ya kiafya katika Ukanda wa Gaza. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Israel unatumia maji safi yanayopatikana katika Ukanda wa Gaza katika kunyunyizia ardhi zake za kilimo.
Uhaba wa madawa na mahitaji ya kiafya ni tatizo jingine muhimu linalowasumbua wakazi wa Ukanda wa Gaza, tatizo ambalo likichanganyika na matatizo mengine tuliyoyazungumzia mwanzoni linaweza kusababisha mkasa  mkubwa wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Hii ni katika hali ambayo idadi ya wagonjwa wanaotatizwa na magonjwa mbalimbali katika ukanda huo imeongezeka sana katika siku za hivi karibuni. Awali shirika la WHO lilitahadharisha kwamba litalazimika kufunga idadi kadhaa ya vituo vyake vya afya katika Ukanda wa Gaza kutokana na kutokuwa na madawa pamoja na vifya vya kutosha vya matibabu. Kutokana uhaba huo idadi kubwa ya wagonjwa wa Gaza tayari wapekwishapoteza maisha yao na wengine wanasubiri tu mauti katika nyumba zao au katika vituo vya afya visivyokuwa na vifaa vyovyote vya kuwatibu.

GAZETI ANNUUR APRIL 19, 2013

ANNUUR 1067 by MZALENDO.NET

KURA ZA VENEZUELA KUHESABIWA TENA


Rais mteule wa Venezuela, Nicolas Maduro, leo amepata uungaji mkono wa viongozi wa mataifa ya Amerika ya Kusini  mjini Lima, kuhusiana na  mipango yake ya kutanuwa ukaguzi wa kura kwa njia ya elektroniki, kama njia ya kuituliza hali ya mambo kutokana na mzozo juu ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili iliopita. Hayo yanafuatia mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Amerika ya Kusini, UNASUR, uliofanyika  kwenye mji mkuu wa Peru, Lima, masaa machache kabla ya mpango wa kuapishwa Maduro mjini Caracas. Maandamano ya upinzani yalizuka nchini Venezuela baada ya Maduro kushinda uchaguzi wa Jumapili kwa kiasi ya asilimia mbili zaidi ya kura za mpinzani wake Henrique Capriles ambaye amedai kura zihesabiwe upya. Tume ya Uchaguzi nchini humo sasa imesema itahesabu tena asilimia 46 ya kura iliyosalia, baada ya awali kuzihesabu tena zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

MATEKA WA KIFARANSA WAACHIWA HURU CAMEROON


Familia ya watu saba raia wa Ufaransa waliotekwa nyara na waasi wa Kislamu miezi miwili iliyopita nchini Cameroon wameachiliwa huru. Ofisi ya rais wa Ufaransa imesema kuwa familia hiyo iko katika afya nzuri na Waziri wa Mambo ya nje Laurent Fabius anaelekea nchini Cameroon kuiona familia hiyo.
Rais  wa Cameroon Paul Biya naye amethibitisha kuachiliwa huru kwa familia hiyo kutoka Ufaransa ambayo ilitekwa nyara na kuwasafirisha nchini Nigeria. Familia hiyo kwa sasa imepata hifadhi katika Ubalozi wa Ufaransa jijini Yaounde nchini humo ikisubiri kurejea nyumbani. Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa serikali yake haikulipa kikombozi kwa waasi hao wa Kislamu waliowateka nyara raia hao wa Ufaransa.
Familia ya raia hao wa Ufaransa walikuwa wanaishi nchini Cameroon tangu mwaka 2011 na walitekwa nyara na kundi la Kiislamu walipokuwa wamekwenda kutalii katika mbuga ya kitaifa ya Waza. Kundi la Boko Haram kutoka nchini Nigeria limekuwa likishukiwa kutekeleza utekwaji nyara huo na kuwaficha raia hao wa Ufaransa.

Friday, April 19, 2013

KATIBU MKUU WA UN AKUTANA NA VIONGOZI WA JESHI LA MAREKANI


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa jeshi la Marekan akiwemo Waziri wa Ulinzi Chuck Hagel na Mkuu wa Vikosi vya Majeshi Yote ya nchi hiyo Martin Dempsey.
Ripoti zinasema kuwa kiini cha mazungumzo hayo kilikuwa mgogoro wa sasa katika peninsula ya Korea na uwezekano wa kupelekwa jeshi la kilinda amani la Umoja wa Mataifa katika nchi za Mali, Somalia na Syria.
Katika mazungumzo hayo Ban Ki-moon ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatari ya kushadidisha mivutano katika peninsula ya Korea kutokana na suutafahumu zilizojitokeza kati ya pande mbilizi zinazozozana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mgogoro mkubwa katika eneo hilo.
Mgogoro katika peninsula ya Korea umeshadidi zaidi kutokana na jitihada za nchi za Magharibi za kutaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lizidishe vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini na vilevile mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini na harakati za kijeshi za Washington ikiwa ni pamoja na kutuma silaha za kisasa huko Seol, Korea Kusini na Tokyo nchini Japan.

KUFELI KWKA IRON DOME KWAITIA KIGUGUMIZI ISRAEL

Duru za habari kutoka Israel, zinaarifu kuwa utawala wa Kizayuni unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, umepatwa na kigugumizi baada ya ngao yake ya makombora ijulikanayo kama 'Kuba  la Chuma' kushindwa kuzuia makombora ya wanamapambano wa Palestina. Hali hiyo imedhihiri baada ya kuanguka makombora katika kitongoji cha Eilat yakitokea eneo la Sinai, Misri. Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Israel ilitangaza ripoti zilizosisitiza kuwa, ilikuwa imeeweka Kuba la Chuma la kuzuia makombora katika mji huo, baada ya kuwepo kwa tishio la kutekelezwa mashambulizi ya makombora. Hata hivyo hapo juzi utawala huo ulitangaza kuwa, rada zake zilikuwa zimegundua makombora yaliyokuwa yanaelekea katika eneo hilo, hali iliyoufanya upige ving'ora vya hatari, huku ngao yake ya makombora ya 'Kuba la Chuma' ikishindwa kufyatua makombora ya kuyazuia makombora hayo. Kufuatia hali hiyo, utawala huo bandia umejitetea kwa kusema kuwa, kuba lake la chuma halikufyatua kombora la kutungua kutokana na sababu za kijografia. Hali hiyo imewafanya walowezi wa Kizayuni kuishi katika hali ya wasiwasi mkubwa baada ya kufahamu kuwa, kuba hilo lililokuwa likipigiwa upatu na Tel Aviv, haliwezi kuzuia kishindo cha makombora ya muqawama unaouzunguka utawala huo bandia.

Thursday, April 18, 2013

KWA FORM FOUR NA FORM SIX . Part 2

Assalamu Alaykum Warahmatul lahi Wabarakatu.

Msamu kama jumuiya ya wanafunzi wa chuo cha Afya Muhimbili tunapenda kuongeza haya machache kwa wanafunzo walio na wanaoingia Form Four na Six. Kwa kuwa jumuiya ni ya wanafunzi wanaosomea Idara ya Afya hivyo basi kuna taarifa nyingi kuhusu masuala ya Kiafya kuanzia masuala ya Vyuo na mengineyo. Hivyo basi kwa wanafunzi wa kozi za Biashara, Arts, na nyinginezo usijione kuwa jumuiya yetu imekusahau. 
Ila ni kuwa inakupa wewe kama mwanafunzi ambaye si wa kozi za Afya njia za kufanya kuweza kutafuta hizo taarifa kwa kozi unayoitaka. Kwa mfano, katika kozi za kiafya Jumuiya imetoa miongozo mbalimbali kama taarifa kwa kozi fulani na vyuo zinapotolewa, kutaarifiana unapofika wakati wa kuapply, au kuweka nakala za baadhi ya  Prospectus (Muongozo au kanuni za chuo) za baadhi ya vyuo. Hii iwe ni sababu kwa yule ambaye si mwanafunzi wa kozi za afya ajue wapi ataweza kutafuta information kwa jili ya kozi anazotaka.

Hivyo basi jumuiya bado inawakaribisha wanafunzi wa level zote za Secondary kuja chuoni Muhimbili kwa ajili ya kupata USHAURI katika masuala mazima ya kusoma na tunafuraha kuwa na wewe katika kukushauri. 

Kufanikiwa kwako wewe basi ni kufanikiwa kwa uislam kwa ujumla. Hivyo uisomapo taarifa hii mfikishie na mwenzoko na mwingine kwani kushikamana kwetu ndio njia ya kuyaelekea mafanikio ya kweli. Kwa mwenye kutaka kuja ofisini kwetu basi afike MSIKITINI (ndani ya Hospitali ya Muhimbili) itafute LIBRARY na kisha ulizie uongozi IDARA YA HABARI.

Pia unaweza wasiliana nasi kupitia TWITTER na uliza maswali  yako au kwa njia ya COMMENTs.

RAIS AUNGA MKONO MSAMAHA KWA BOKO HARAM


Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amezindua kamati mpya itakayochunguza uwezo na utekelezwaji wa msahama kwa kundi la wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram. Kamati hiyo itakuwa na siku sitini kufikia uamuzi wake wa mazungumzo na kuwapokonya silaha wapiganaji hao , kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ofisi ya rais. Pia itaangazia nyenzo za kuwasaidia waathiriwa wa ghasia ambazo chanzo chake ni wapiganaji hao. Boko Haram limewaacha maelfu wakiwa wamefariki kutokana na ghasia ambazo wamekuwa wakisababisha mara kwa mara tangu mwaka 2009.
Kamati hiyo ambayo wanachama wake 25 wanajumuisha maafisa wa kijeshi, wasomi na wanasiasa watajaribu kuangazia sababu zinazopelelea makundi kama Boko Haram kuafanya uasi na njia za kuwazuia. Zaidi ya hayo, rais Jonathan ameidhinisha kuundwa kwa kamati nyingine ya serikali kuhusu kuwapokonya wapiganaji hao silaha katika jitihada zake za kuimarisha usalama na uthabiti wa nchi. Viongozi wa kisiasa na kidini, kutoka Kaskazini mwa Nigeria, ambalo ndio kitovu cha uasi huo, hivi karibuni walipendekeza serikali kutoa msamaha kwa wapiganaji hao.
Rais Goodluck Jonathan alijibu kauli hiyo na mwanzoni mwa mwezi Aprili alikipa kikundi cha washauri wa usalama jukumu la kuangalia ambavyo msamaha unaweza kutolewa kwa wapiganaji hao. Duru zinasema kuwa hoja hii ya msamaha ni muhimu kwani rais alikuwa ameipuuza mwanzoni. Ni wazi kuwa rais ameitikia kuwa juhudi za kijeshi dhidi ya wapiganaji hao hazijazaa matunda. Hata hivyo haijulikani ambavyo wapiganaji hao watatizama wazo la rais ikizingatiwa kuwa ni makundi mengi ya mirengo tofauti ya wapiganaji. Wiki jana Boko Haram, ambao wanataka utawala wa kiisilamu Kaskazini mwa nchi limekataa pendekezo la msamaha kwao.

NETANYAHU ASEMA ISRAEL INA HAKI YA KUZUIA SILAHA KWENDA SYRIA


Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema, Israel ina haki ya kuzuia silaha kuishia kwenye mikono ya wapiganaji wa kiisilamu nchini Syria. Akiongea na BBC, Bwana Netanyahu ameonya silaha za kudungua ndege na makombora zinaweza kubadilisha mashariki ya kati na kuifanya uwanja wa magaidi na kuhatarisha usalama wa dunia. Bwana Netanyahu yuko mjini London wakati Uingereza inapendekeza marufuku ya silaha iliyowekewa Syria na bara Ulaya kuondolewa. Uingereza inataka wapiganaji nchini Syria kupokea silaha.
Japo Netanyahu anaunga mkono hatua hiyo, anaonya huenda silaha zikaishia kwenye mikono ya wanamgambo wa kiisilamu na kuhatarisha hali zaidi ya ilivyo kwa sasa. Amesema wasi wasi wa Israel ni silaha zilizoko ndani ya Syria, zikiwemo makombora ya kudungua ndege ambayo ni hatari endapo yataishia kwenye mikono ya magaidi.
Waziri Mkuu wa Israel hata hivyo amesema nchi yake haina mpango wa kushambulia Syria, japo amesisitiza kua Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya mashamblizi. Israel ina wasi wasi kuhusu kundi la Nusra Front liliko Syria na ambalo limekiri kua na uhusiano na mtandao wa Al Qaeda. Netanyahu amesema wasi wasi wake siyo kwa Israel pekee bali ni kwa dunia nzima.

KOREA KASKAZINI YATAKA VIKWAZO VIONDOLEWE

Korea Kaskazini imedai kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia pamoja na majaribio yake ya makombora. Pia nchi hiyo inataka ahadi kutoka kwa Marekani kutoshiriki kile imekitaja kuwa ni "kitendo cha vita vya nyuklia" na Korea Kusini, kama kweli Marekani inataka paweko mazungumzo. Masharti hayo mapya yamekuja wakati kukiwa na hofu kuhusiana na uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora. Mazungumzo yanayozihusisha pande sita, yaani Korea Kaskazini na Kusini, Japan, Marekani, Urusi na China yalikwama mnamo mwaka wa 2009. Rais wa Korea Kusini Park Guen Hye ameialika Korea Kaskazini katika meza ya mazungumzo ili kupunguza mvutano ambao umeongezeka kuhusiana na wasiwasi kuwa serikali ya Kaskazini inapanga kufyatua kombora. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry wameitaka Korea Kaskazini kurudi katika meza ya mazungumzo.

MRIPUKO MKUBWA WATOKEA KIWANDA CHA MBOLEA TEXAS, MAREKANI

Zaidi ya watu 200 wamejeruhiwa na wengine wengi wanahofiwa kuuawa kutokana na mlipuko mkubwa katika kiwanda cha mbolea katika jimbo la Texas nchini Marekani. Ripoti za mwanzo zinasema watu wawili wamethibitiwa kufariki lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Juhudi zinaendelea za kuwatafuta watu waliokwama katika nyumba zao. Maafisa wamesema mlipuko huo uliotokea jana usiku katika kiwanda cha West Fertilizer Plant umeharibu kabisa majengo kadhaa karibu na eneo hilo. Mlipuko huo ulitokea wakati wazima moto wa kujitolea walipokuwa wakijaribu kuuzima moto katika kiwanda hicho. Wafanyakazi wa huduma za matibabu wameweka kituo cha matibabu katika eneo la mkasa, wakati watu wakihamishiwa maeneo salama kwa hofu ya kupumua hewa ya sumu. Maafisa wanasema kati ya nyumba 50 na 75 zimeharibiwa kabisa kutokana na milipuko hiyo.

MAHAKAMA PAKISTAN YAAMURU KUKAMATWA MIUSHARAF

Mahakama moja nchini Pakistan leo imeamuru kukamatwa kiongozi wa zamani wa kijeshi Pervez Musharraf kuhusiana na uamuzi wake wenye utata wa kuwafuta kazi majaji wakati alipotangaza sheria ya hali ya hatari mnamo mwaka wa 2007. Haijabainika wazi ikiwa  jenerali huyo mstaafu atakamatwa. Musharraf aliondoka katika mahakama ya Islamabad, bila kuzuiwa na mafisa wa usalama waliokuwa wamejaa nje ya mahakama, na kuondoka ndani ya gari lake akisindikizwa na walinzi wake. Msemaji wa chama chake amesema kiongozi huyo atawasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kupinga amri ya kukamatwa kwake. Musharraf anakabiliwa na mashitaka ya kupanga njama ya mauwaji ya kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto mwaka wa 2007, na kuhusiana na kifo cha kiongozi wa waasi kabila la Baluch wakati wa operesheni ya kijeshi mwaka wa 2006. Rais huyo wa zamani alirudi nyumbani tarehe 24 mwezi uliopita,baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka minne nchini Dubai na Uingereza, na kuahidi kugombea katika uchaguzi mkuu.