MELI YA KIVITA YA IRAN YATIA NANGA SUDAN
Meli ya kivita ya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetia nanga katika bandari ya Sudan katika Bahari Nyekundu.
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran Admeli Habibollah Sayyari amesema manowari hiyo ijulikanayo kama 'Jamaran' na ambayo imetengenezwa kikamilifu nchini Iran imewasili Sudan ikiwa na ujumbe wa amani na kirafiki kwa nchi za eneo na rafiki.
Manowari hiyo ni sehemu ya msafara wa 23 wa Jeshi la Wanamaji la Iran uliotumwa katika Bahari Nyekundu. Msafara wa 22 wa manowari za kivita za Iran ulirejea nchini mapema mwezi huu baada ya kumaliza kazi ya siku 75 katika maji ya kimataifa.
Jeshi la wanamaji la Iran limeimarisha harakati zake katika maji ya kimatiafa kwa lengo la kulinda doria na kusindikiza meli za Iran na za kigeni katika maji hayo. Katika fremu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na maharamia, Jeshi la Wanamaji la Iran limekuwa likilinda doria katika Bahari Hindi na Ghuba ya Aden tokea Novemba mwaka 2008.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya bahari IMO limepongeza juhudi na mafanikio ya Iran katika kupambana na maharamia.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO