Friday, November 30, 2012

PALESTINA YAWA NCHI MTAZAMAJI WA UN



Palestina imekubaliwa kuwa nchi mtazamaji asiyekuwa mwanachama katika Umoja wa Mataifa.
Katika kura iliyofanyika jana kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Palestina ilifanikiwa kupata kura 138 za ndio mkabala wa kura 9 zilizopinga Palestina kuwa nchi mtazamaji katika Umoja wa Mataifa.
Matokeo hayo yamepandisha juu nafasi na hadhi ya Palestina ambapo sasa inatambuliwa kuwa ni nchi mtazamaji katika Umoja wa Mataifa badala ya jumuiya mtazamaji katika jumuiya hiyo ya kimataifa.
Habari hiyo ya kutambuliwa Palestina kuwa ni nchi mtazamaji badala ya jumuiya katika Umoja wa Mataifa imezusha furaha, vifijo na nderemo huko Palestina. Hatua hiyo inaipa Palestina fursa ya kushiriki katika vikao vya Umoja wa Mataifa na kuboresha uanachama wake katika taasisi za umoja huo.
Mwaka 2011 Wapalestina waliomba kutambuliwa rasmi kama nchi mwanachama katika Umoja wa Mataifa lakini ombi hilo halikufanikiwa kutokana na upinzani wa Marekani na waitifaki wake.
Mara hii pia Marekani pekee kati ya nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imepinga suala la kupewa Palestina sifa ya nchi mtazamaji huku Uingereza ikikataa kupiga kura.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO