Tuesday, December 18, 2012

AU BAADA YA KIFO CHA GHADAFI, BAJETI HAITOSHI


Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bi. Nkosazana Dlamini Zuma amesema kuwa umoja huo unasumbuliwa na upungufu wa bajeti ya matumizi yake. Bi. Zuma amesema Umoja wa Afrika (AU) unataka kuelekea kwa wafadhili wapya kwa ajili ya kutafuta fedha za kudhamini bajeti yake badala ya kuendelea kutegemea nchi wanachama. Zuma amesisitiza kuwa moja ya malengo ya AU ni kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika kuwekeza barani humo na kuzidisha mabadilishano ya kibiashara na nchi za Kiafrika.

Kwa kawaida bajeti ya Umoja wa Afrika hudhaminiwa na nchi wanachama. Kwa sasa Benki ya Afrika na Kamisheni ya Uchumi ya Afrika katika Umoja wa Mataifa zina nafasi muhimu katika kudhamini gharama za matumizi ya AU.
Pamoja na hayo matatizo ya kifedha ya Umoja wa Afrika yangali palepale na yanahesabiwa kuwa moja na nakisi kubwa za jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Afrika. Kabla ya kung'olewa madarakani dikteta wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, nchi hiyo ilikuwa mdhamini mkubwa wa bajeti ya Umoja wa Afrika na kwa msingi huo AU imepoteza mmoja wa wadhamini wakuu wa bajeti yake baada ya kung'olewa kwake madarakani.
Ripoti zinasema kuwa bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka wa fedha wa 2012 ni dola bilioni mbili na milioni mia mbili na 12. Umoja huo wa Afrika una nafasi kubwa katika kupunguza utegemezi wa nchi wanachama na kulinda mipaka ya nchi za Afrika iliyokuwepo wakati nchi hizo zinapata uhuru. Vilevile jumuiya hiyo ina mchango mkubwa na majukumu mazito ya kutekelea siasa za ulinzi wa pamoja barani Afrika na kutatua migogoro na ugomvi unaotokea baina ya nchi wanachama.
Mambo mengine yanayopewa kipaumbele katika siasa za Umoja wa Afrika ni kufanya jitihada za kuzuia uingiliaji wa nchi yoyote katika masuala ya nchi mwanachama, kutekeleza maamuzi ya jumuiya hiyo katika masuala mazito kama yale yanayohusiana na jinai za kivita, mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu, kutoa misaada katika operesheni za kurejesha amani na kusimamia utekelezaji wa demokrasia na utawala wa sheria. Wataalamu wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kuanza mahusiano mpya ya kimataifa baada ya kipindi cha vita baridi kumeleta fremu mpya ya ushirikiano wa Afrika na nchi nyingine za dunia zikiwemo nchi zilizopiga hatua kiviwanda.
Ala kulli hal, majukumu na kazi nzito ya Umoja wa Afrika yanailazimu jumuiya hiyo kubwa ya Kiafrika kuwa na bajeti ya kutosha ili iweze kutekeleza vyema mipango yake na kufikia malengo yanayokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO