Japan imeziamuru ndege zake za kivita zipae angani baada ya
ndege ya serikali ya Uchina kuingia katika anga ya visiwa vya Bahari ya
Mashariki mwa Uchina kwa muda, duru rasmi zimesema. Msemaji wa serikali Osamu
Fujimura alisema kuwa Japan iliamuru ndege za kivita za aina ya F-15 zipae
angani wakati ndege hiyo ya Uchina ilipoonekana.Tukio hilo lilipotokea tu,
Japan "iliilalamikia" Uchina “mara moja”, shirika la habari la Kyodo
lilimnukuu akisema. Visiwa hivyo, vinavyojulikana kama Senkaku nchini Japan na
Diaoyu nchini Uchina, vimegombaniwa na nchi hizo mbili kwa muda mrefu sasa.
Walinzi
wa baharini wa Japan nao pia walisema kwamba meli za Uchina zinazofanya
uchunguzi nazo zilionekana karibu na visiwa hivyo mapema siku hiyo. Kwa upande
wake, Uchina imesema kwamba safari ya ndege yake hiyo ni jambo la kawaida. Japan
ndiyo inayomiliki visiwa hivyo, ambavyo pia Taiwan inadai ni vyake. Bahari
inayozunguka visiwa hivyo ina samaki wengi na pia inadhaniwa kwamba ina mafuta.
Japan ilitwaa visiwa vitatu kutoka kwa mmiliki Mjapani wa kibinafsi mnamo mwezi
Septemba, lakini kitendo hicho kilizua malalamishi ya kidiplomasia na kutoka
kwa raia nchini Uchina. Tangu hapo, meli za Kichina zimekuwa zikionekana katika
eneo la visiwa hivyo, jambo ambalo limeisababisha Japan kutoa onyo mara kwa
mara.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO