Waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamemtaka Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo ang’atuke madarakani.
Hayo yamesemwa na kiongozi wa kundi hilo Askofu Jean-Marie Runiga na kuongeza kuwa, makundi mbalimbali ya kisiasa nchini yatawasilisha maombi yao kwa serikali ya Kinshasa na kutoa wito wa kuuzuliwa Kabila. Waasi wa M23 waliuteka mji wa mpakani wa Goma, baada ya majeshi ya Umoja wa Mataifa kusimamisha mapigano katika mji huo. Hata hivyo walikubali kurejea nyuma kutoka kwenye maeneo waliyokuwa wameyateka, baada ya kukubali kufanya mazungumzo na serikali ya Kinshasa. Goma ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini na una wakaazi wapatao milioni moja. Katika upande mwingine Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye ni mpatanishi kati ya serikali na waasi wa M23 Crispus Kiyonga amesema, mazungumzo yaliyoakhirishwa kati ya pande mbili yataendelea mwakani. Hata hivyo amesema kuwa, mazungumzo hayo licha ya kupiga hatua kubwa, lakini bado yanakabiliwa na changamoto nyingi.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO