OBAMA AMUONYA ASSAD
Rais wa Marekani Barack Obama ameionya serikali ya Syria kuwa matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya watu wake hayatakubaliwa na yatasababisha matokeo mabaya kwa nchi hiyo. Rais Obama ametoa onyo hilo, huku kukiwa na wasiwasi kwamba vikosi vya Syria vinachanganya kemikali za sumu kwenye silaha zake. Katika taarifa nyengine, duru za kidiplomasia zinasema kwamba msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Syria Jihad Maqdisi ameondoka serikalini na kuikimbia nchi hiyo. Maqdisi alizungumzia kuhusu silaha za kemikali mwezi Julai mwaka huu, akisema kwamba zisingetumika dhidi ya raia. Wakati hali kuzunguka mji wa Damascus inazidi kuwa mbaya, Umoja wa Mataifa unajitayarisha kuwaondoa wafanyakazi wake wasio muhimu kutoka nchini humo. Wakati huo huo mshirika wa karibu wa serikali ya Syria , Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa nchini Uturuki jana kwa mazungumzo ya kibiashara na kuijadili hali nchini Syria.
Uturuki inaunga mkono upinzani nchini Syria na imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya Rais Bashar al-Assad.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO