THE HAGUE KUSIKILIZA MASHITAKA YA WAPALESTINA
Baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
kupandisha hadhi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa na kuwa nchi mtazamaji
asiyekuwa mwanachama rasmi, sasa mahakama ya The Hague huko Uholanzi imetangaza
kuwa itaanza kushughulikia mashtaka yaliyowasilishwa na Wapalestina dhidi ya
utawala ghasibu wa Israel.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya
The Hague imetangaza kuwa, hivi karibuni itachunguza suala la kupandishwa hadhi
ya Palestina katika Umoja wa Mataifa na kushughulikia mashtaka ya Wapalestina
kuhusu jinai zilizofanywa na askari wa Israel katika vita vya siku 22 dhidi ya
watu wa Gaza.
Mwaka 2009 Wapalestina waliwasilisha mashtaka
rasmi katika Mahakama ya Jinai ya Kimataifa ya The Hague wakiitaka ichunguze
jinai zilizofanywa na jeshi la Israel katika vita vya siku 22 huko Gaza. Hata
hivyo mashtaka hayo yalikataliwa na mahakama ya The Hague kwa kuwa wakati huo
Palestina ilikuwa bado haijatambuliwa rasmi kuwa nchi mtazamaji katika Umoja wa
Mataifa.
Kwa msingi huo tangu sasa Mahakama ya Kimataifa
ya Jinai itakuwa na uwezo wa kisheria wa kuchunguza na kushughulikia mashtaka
yote yanayowasilishwa na Wapalestina. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, nchi
ndizo zinazoweza kuwasilisha mashtaka katika Mahakaya ya Kimataifa ya The Hague.
Kabla ya uamuzi wa tarehe 29 Novemba wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao
uliitambua Palestina kuwa ni nchi mtazamaji, hapakuwepo uwezekano wa kusikilizwa
mashtaka ya Wapalestina dhidi ya Israel.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana utawala ghasibu
wa Israel na waitifaki wake wakubwa hususan Marekani wakafanya jitihada kubwa za
kukwamisha suala la kutambuliwa Palestina kuwa ni nchi japo isiyo mwanachama
katika Umoja wa Mataifa.
Katika mkondo huo huo Rais wa Mamlaka ya Ndani ya
Palestina Mahmoud Abbas alitangaza baada tu ya kurejea Ramallah akitokea New
York kwamba, Quds Tukufu ndio mji mkuu wa milele wa nchi ya Palestina. Alisema
sasa Wapalestina wamepata nchi na wanaweza kuwasilisha matakwa yao halali katika
jamii ya kimataifa. Abbas aliashiria mashinikizo makali yaliyofanyika kwa
shabaha ya kuzuia suala la kutambuliwa Palestina kuwa ni nchi mtazamaji katika
Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, karibu asilimia 75 ya jamii ya kimataifa
imewapigia kura ya ndio watu wa Palestina.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema
kuwa mafanikio hayo yatabadilisha mlingano wa nguvu za kisiasa katika Mashariki
ya Kati.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO