Wednesday, December 05, 2012

UN: MITAMBO YA NYUKLIA YA ISRAEL LAZIMA IKAGULIWE


Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa wingi wa kura azimio linaloutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uandae mazingira haraka iwezekanavyo ya kuingia wakaguzi wa umoja huo huko Israel kwa shabaha ya kukagua mitambo ya nyuklia ya utawala huo ghasibu.
Taarifa zinaeleza kuwa, kamati ya upokonyaji silaha ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia imetangaza uungaji mkono wake kwa mkutano ulioakhirishwa hivi karibuni wa kuzuia la silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati. Nchi zote za Kiarabu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilitangaza azma zao za kushiriki kwenye mkutano huo uliopangwa kufanyika katikati ya mwezi huu wa Disemba katika mji wa Helsinki nchini Finland. Hata hivyo tarehe 23 Novemba Marekani ilitangaza kuakhirishwa mkutano huo hadi siku nyingine kwa kisingizio cha kukosekana utulivu wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa jana limeutaka utawala wa Israel ujiunge haraka iwezekanavyo na makubaliano ya kuzuia uzalishaji na utumiaji silaha za nyuklia NPT sambamba na kufungua milango kwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukagua mitambo ya nyuklia ya Israel.
Nchi za Kiislamu za eneo la Mashariki ya Kati zinaeleza kuwa, mitambo ya nyuklia ya utawala wa Israel ndiyo tishio kubwa la amani na uthabiti katika eneo hili, kwani utawala huo unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya nyuklia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO