Sunday, December 16, 2012

UFARANSA WARUDISHA MAJESHI TOKA AFGHANISTAN

Ufaransa leo imewaondoa wanajeshi wake wa mwisho wa mapigano nchini Afghanistan, ikiwa ni miaka miwili kabla ya nchi washirika katika ujumbe wa NATO wenye wanajeshi laki moja zikiongozwa na Marekani kuviondoa vikosi vyao nchini humo. Takribani wanajeshi 200 wa kitengo kilichoshughulika na mipango wa kuharakisha kuondolewa kwa vikosi vya Ufaransa kutoka katika vita vilivyodumu miaka 11, kimeondoka leo nchini Aghanistan. Wanatarajiwa kurejea nyumbani Ufaransa Desemba 18 baada ya siku tatu za mapumziko nchini Cyprus. Kuondoka kwao huko kunamaanisha kuwa Ufaransa sasa ina takriban wanajeshi 1,500 waliobakia nchini Afghanistan, wengi wao katika mji mkuu Kabul. Wanatarajiwa kusalia nchini humo mwaka ujao huku wakiwajibika na mipango ya kuvirejesha nyumbani vifaa na kuwapa mafunzo wanajeshi wa Afghanistan, ili kuchukua majukumu ya usalama wa taifa. Mapema leo Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema wanajeshi wa Marekani na Jumuiya ya NATO wanaokabidhi mamlaka ya usalama kwa majeshi ya Aghanistan wanapaswa kuondoka katika vijiji vya Afghanistan haraka iwezekanavyo na kurudi kambini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO