Monday, December 17, 2012

WAPINZANI WA MISRI BADO WAYAPINGA MATOKEO MAPYA

Wapinzani nchini Misri wamekataa kutambua matokeo ya kura ya maoni ya katiba iliyofanyika siku ya Jumamosi na badala yake wametoa wito wa kufanyika maandamano ya kulalamikia kile walichokitaja kuwa udanganyifu uliogubika kura hiyo ya maoni. Muungano wa wapinzani unaojulikana kwa jina la Kambi ya Wokozi wa Kitaifa Misri umetoa wito wa kufanyika maandamano ya nchi nzima hapo kesho kulalamikia zoezi hilo la kura ya maoni ya katiba mpya.

 Taarifa ya Kambi ya Wokozi wa Kitaifa imewataka Wamisri kujitokeza kwa wingi hiyo kesho kwa ajili ya kutetea uhuru na kuzuia wizi wa kura. Siku ya Jumamosi wananchi wa Misri walishiriki katika awamu ya kwanza ya kura ya maoni ya katiba mpya ya nchi hiyo ambapo matokeo yanaonyesha kuwa, asilimia 56.5 ya washiriki wa kura hiyo ya maoni waliipigia kura ya ndiyo rasimu hiyo ya katiba. Wakati huo huo, Kamisheni Kuu ya Uchaguzi ya Misri imepinga wito wa wapinzani wa kutaka kurejewa zoezi la kura hiyo ya maoni na kusisitiza kwamba, hakukuweko na kasoro ambazo zinaweza kuwa na taathira katika matokeo ya kura hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO