Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefanya ziara ya kushitukiza nchini Libya hivi leo, ziara inayokuja siku chache baada ya Uingereza kutoa tahadhari kuhusu vitisho vinavyoukabili ubalozi wake mjini Tripoli. Cameron amewasili mchana wa leo huku kukiwa na ulinzi mkali. Akiongozana na waziri wa mambo ya ndani wa Libya Ashur Shwayel, Cameron alikwenda moja kwa moja katika chuo cha mafunzo ya polisi kusini mwa mji mkuu Tripoli, ambako alihudhuria sherehe ya kupandishwa vyeo kwa maafisa wa polisi. Maafisa wa serikali ya Libya wameliambia shirika la habari la AFP kuwa ushirikiano katika nyanja ya usalama utakuwa katika ajenda ya juu katika mazungumzo baina ya Cameron na maafisa wa Libya. Ofisi ya waziri mkuu mjini London imesema kuwa Cameron amekwenda nchini Libya kujadiliana juu ya namna Uingereza inavyoweza kuendelea kusaidia ujenzi wa Libya imara, yenye maendeleo na demokrasia.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO