Kundi kubwa la magari ya deraya na magari mengine yaliyobeba askari wa Chad
kuelekea nchini Mali, limewasili mji mkuu wa Niamey nchini Niger. Vikosi hivyo
vya Chad vinaelekea nchini Mali kwa ajili ya kushiriki katika oparesheni za
kijeshi dhidi ya waasi wa nchi hiyo wanaoyadhibiti maeneo ya kaskazini. Kwa
mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya Chad, vikosi hivyo vitaweka kambi
katika mji wa Ouallam uliopo umbali wa kilometa 100 kaskazini mwa mji mkuu wa
Niger, Niamey. Askari wa Niger wapatao 500 wapo katika eneo la mpakani. Hii ni
katika hali ambayo, hadi sasa Chad ina wanajeshi wapatao 400 huko Niger.
Hatimaye askari wa Chad na Niger wataelekea nchini Mali na kupiga kambi katika
mji wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo. Utumwaji wa askari hao unafanyika chini ya
mwamvuli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (Ecowas) iliyopitisha
azimio la kutumwa askari wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wapatao 3300 huko
nchini Mali kwa ajili ya kuwatokomeza waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO