Friday, January 25, 2013

UFARANSA YAHARIBU VITUO VYA WAASI WA MALI

Ndege za kivita za Ufaransa zimeviharibu vituo viwili vya wapiganaji wa Kiislamu kaskazini mwa Mali, wakati ambapo kuna ripoti kuwa waasi hao wamegawanyika katika makundi mawili, moja likitaka kufanya mazungumzo ili kukomesha mashambulizi dhidi yao. Pia kumekuwepo na taarifa za majeshi ya Mali kufanya mauaji ya kinyama, ambapo kundi moja la haki za binaadamu limesema kuwa watu wasiyopungua 31 waliuawa katika mji wa kati wa Sevare, na maiti zao kutupwa katika visima. Chanzo kutoka duru za jeshi kimesema kuwa mashambulizi ya ndege yaliyofanyika usiku yamelenga vituo vilivyoko Ansongo, kilomita 80 kutoka mji wa Gao, na vituo vya kijeshi vya waasi vilivyoko katika kijiji jirani cha Seyna Sonrai. Jana Alhamisi, kundi jipya lililojitenga na Ansar Deen la Islamic Movement for Azawad, lilisema katika taarifa yake kuwa linapinga itikadi kali na ugaidi, na kwamba limedhamiria kupambana navyo, na kuongeza kuwa linataka suluhu ya muafaka ya mgogoro huo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO