Wednesday, January 23, 2013

MAREKANI KUTUMA WANAJESHI 3500 NCHI ZA AFRIKA

Serikali wa Marekani imeazimia kupeleka wanajeshi 3,500 katika nchi 35 za Kiafrika mwaka huu wa 2013. Gazeti la World Tribune linalochapishwa Marekani limeandika kuwa, hatua hiyo ya Washington ina shabaha ya kukabiliana na ongezeko la nguvu za kundi la al Qaeda na vitisho vya makundi mengine yenye mfungamano na kundi hilo. Gazeti hilo limeandika kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon imesisitiza juu ya kutumwa majeshi hayo kwenye maeneo yaliyokumbwa na ghasia barani Afrika kwa lengo la kutokomeza ugaidi.
Jenerali Carter Ham Kamanda wa Majeshi ya Marekani barani Afrika AFRICOM amesema kuwa, hali iliyoko hivi sasa Afrika inatofautiana na ilivyokuwa hapo awali. Jenerali Ham ameongeza kuwa, kuna makundi mapya yanayobeba silaha ambayo hayana uhusiano na mtandao wa al Qaeda na kusisitiza kuwa, makundi hayo ni tishio kubwa kwa Marekani. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, Marekani bado inatumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kwa lengo la kuimarisha satua zake na kufikia malengo yake haramu katika maeneo mengi duniani

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO