Wabunge nchini Marekani wameshindwa kutatua mkwamo wa bajeti kwa wakati uliopangwa hapo jana lakini wanaendela na mazungumzo ili kulinusuru taifa hilo na madhara yatokanayo na ongezeko kubwa la kodi. Katika juhudi za kupambana na hali hiyo wakati huu wa sherehe za mwaka mpya, wabunge wa chama cha Republican na ikulu ya nchi hiyo, walifikia makubaliano ambayo yanamaanisha kuwa Wamarekani wenye kipato kikubwa tu ndiyo watakaguswa na ongezeko la kodi lakini bado tatizo limebakia katika namna ya kupunguza matumizi ya serikali kwa kiasi cha dola bilioni 109. Licha ya makubaliano hayo, kitaalamu uchumi wa nchi hiyo umeingia kwenye mkwamo usiku wa manane jana baada ya viongozi wa chama cha Republican kusema hakuna kura itakayopigwa kuhusu makubaliano hayo. Hata hivyo Baraza la Seneti bado lina matumaini kuwa kura huenda ikapigwa majira ya usiku ikiwa mpango huo utakamilika. Kitaalamu ongezeko la kodi na mpango wa kubana bajeti vinaanza leo tarehe Mosi Januari, lakini viongozi hao wana muda wa saa chache nyengine kabla ya makali kuanza kwa kuwa masoko ya fedha hayafanyi kazi leo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO