Saturday, January 12, 2013

MAREKANI YAZIDISHA HARAKATI ZA MAKUBALIANO YA PALESTINA NA ISRAEL

Duru za habari zinaripoti kuwa Marekani imezidisha harakati zenye lengo la kuyafufua mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba David Hale, mjumbe maalumu wa Washington katika Mashariki ya Kati anafanya safari katika eneo ili kuandaa mazingira ya kuanzisha tena mazungumzo hayo. Duru za kisiasa za Palestina zinalielezea lengo la safari ya David Hale hapa Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ni kufanya mashauriano juu ya mpango mpya wa Marekani wenye madhumuni ya kuufufua mwenendo wa mazungumzo ya mapatano baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala haramu wa Kizayuni. Itakumbukwa kuwa duru mpya ya mazungumzo ya mapatano baina ya pande hizo mbili kwa usimamizi wa Marekani ilianza tena mwaka 2010, lakini miezi michache baadaye mazungumzo hayo yalivunjika kutokana na ukorofi wa utawala wa Kizayuni ukiwemo wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina. Nukta ya kuzingatiwa katika hali ya sasa ni kwamba kabla ya mazungumzo ya David Hale na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, mamlaka hiyo imeeleza bayana kuwa iko tayari kuanzisha tena mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni. Mwenendo huo unadhihirisha wazi kuwa kufanya mapatano na Wazayuni ndio sera kuu ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo yenyewe imeasisiwa kupitia mchakato huo wa mapatano. Ajabu ni kwamba Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayoongozwa na Mahmoud Abbas inaonyesha kuwa na hamu ya kupatikana maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina lakini kutokana na kufuata njia ya mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni inazidi kudhihirisha mbele ya Wapalestina sura yake halisi ya kuwa kibaraka na tegemezi kwa Wamagharibi. Harakati mpya za Marekani za kufufua mwenendo wa mapatano katika Mashariki ya Kati zinashuhudiwa katika hali ambayo kuna taarifa za kupamba moto vuguvugu la Intifadha ya wananchi wa Palestina na kuanza hivi karibuni Intifadha ya Tatu ya wananchi hao suala ambalo limewatia kiwewe na wasiwasi mkubwa viongozi wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni. Katika miaka ya hivi karibuni umeshuhudiwa muelekeo wa kushtadi hisia za chuki dhidi ya utawala wa Kizayuni na moyo wa muqawama miongoni mwa wananchi wa Palestina ambao umepelekea kushindwa na kupata vipigo vya mtawalia utawala huo ghasibu unaoungwa mkono kwa hali na mali na Magharibi. Kwa sababu hiyo utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wamekuwa wakitumia kila mbinu na hila ikiwemo ya mazungumzo ya mapatano ili kuwafanya wananchi wa Palestina wasiendeleze muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni; na kwa kuidhoofisha Intifadha kuzuia uendelezaji mapambano sambamba na kuviza mafanikio waliyopata Wapalestina hadi sasa kwa ajili ya kufikia malengo yao matukufu. Lakini si hayo tu, bali lengo jengine linalofuatiliwa na utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kupitia harakati mpya za kuhuisha mchakato wa maptano ni kuzusha mpasuko na mfarakano ndani ya safu za Wapalestina ili kudhoofisha nafasi yao katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Na ndiyo maana wakati duru mpya ya mazungumzo ya kufanikisha maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina imeanza, huku Khalid Mash’al, Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wameelekea huko Misri kwa madhumuni hayo, Marekani na utawala wa Kizayuni nazo pia zimeshadidisha njama zao za kufelisha maridhiano hayo ya kitaifa ya Wapalestina. Mamlaka ya Ndani ya Palestina na madola ya Magharibi yanashikilia kuendeleza mchakato wa mapatano katika hali ambayo mchakato huo haujawa na tija nyengine hadi sasa ghairi ya kuujusurisha na kuufanya utawala haramu wa Israel uwe na kiburi kikubwa zaidi cha kuendeleza jinai na sera zake za kujitanua dhidi ya Wapalestina. Matukio ya Palestina yanadhihirisha wazi kuwa Wapalestina wangali wanakabiliwa na njama za pamoja za utawala wa Kizayuni na Marekani, na kwamba mshikamano na kuendeleza Intifadha chini ya mhimili wa muqawama ndio njia pekee itakayowawezesha wananchi hao madhulumu kuzima njama hizo za hila, ghilba na ulaghai zinazotekelezwa na Tel Aviv na Washington

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO