Saturday, January 19, 2013

SUALA LA UCHUMI LATAWALA UCHAGUZI ISRAEL


Siku nne tu zimebakia hadi kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati wake wa bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel. Tarehe 22 mwezi huu, Wazayuni watashiriki kwenye uchaguzi wa bunge la utawala wa Kizayuni huku daghadagha na wasiwasi wao mkubwa ukiwa ni masuala ya kiuchumi na kupanda vibaya gharama za maisha. Uchaguzi huo wa Bunge umegubikwa kikamilifu na mgogoro wa kiuchumi unaowatesa wakazi za ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni unaonesha kuwa asilimia 60 ya wapiga kura katika uchaguzi huo wana wasiwasi mkubwa wa kuzidi kuharibika hali zao za kiuchumi. Kupanda kupindukia gharama za maisha, ukata, mfumumko mbaya wa bei, ukosefu mkubwa wa kazi na hali mbaya ya kijamii na kuenea ufuska na ufisadi ndani ya taasisi za serikali na kati ya wanasiasa wa utawala wa Kizayuni ndiyo matunda yaliyoletwa na Baraza la Mawaziri la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa hivi sasa wa utawala wa Kizayuni. Hali ni mbaya kiasi kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumejitokeza mirengo na harakati nyingi za kuupinga utawala wa Kizayuni katika miji mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ikiwa ni pamoja na maandamano ya mamia ya maelfu ya watu. 
Wazayuni 12 wamejichoma moto na watatu kati yao wamepoteza maisha kwa kujichoma moto katika kipindi hiki ya miaka mitatu iliyopita. Takwimu rasmi zinaonesha kuwa kati ya kila watu wanne wa jamii ya watu milioni sita wa Israel anaishi chini ya mstari wa umaskini huku tabaka la watu wa kati nalo likikabiliwa na mashinikizo mengi ya kifedha. Kwa makumi ya miaka, Wazayuni walikuwa wanazitaja ardhi za Palestina wanazozikalia kwa mabavu kuwa ni ardhi iliyoahidiwa ya mito ya maziwa na asali, lakini hivi sasa utawala uliofilisika kisiasa, kiuchumi na kijamii wa Kizayuni unaonekana umefika mwisho wa njia na hata unashindwa kuzuia kuporomoka mtawalia mabaraza yake ya mawaziri na kuvunjika mabunge yake. Hii ni kwa sababu tangu mwaka 1994 hadi hivi sasa hakuna serikali yoyote ya utawala wa Kizayuni iliyoweza kumaliza salama miaka yake minne bali mara zote mabunge yamekuwa yakivunjwa na mabaraza ya mawaziri yamekuwa yakisambaratika ovyo. 
Kitu ambacho kimekuwa kikiufanya utawala wa Kizayuni uendelee kuwepo katika kipindi chote hiki cha miongo sita ya uhai wa donda hilo la kensa katika kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu ni dola za Kimarekani zinazotoka kwa Wazayuni wa nchi hiyo. Kila mwaka Bunge la Congress la Marekani pekee linatenga dola bilioni 3 za msaada usio na masharti kwa ajili ya kuuendesha kiuchumi na kijeshi utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kuufanya utawala huo kuwa ni tawi la kisiasa na kijeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Kitendo hicho kwa kweli kimewafanya wananchi wa Marekani washindwe kuvumilia na wamekuwa wakifanya maandamano mara kwa mara kulalamikia siasa mbovu za serikali zao. Maandamano makubwa ya "Harakati ya Asilimia 99" ni mfano wa wazi wa jambo hilo. 
Alaakullihaal, zile ndoto za ardhi iliyoahidiwa ya mito ya maziwa na asali walizokuwa nazo Wazayuni zimejithibitisha zenyewe kuwa si kitu kingine ghairi ya ngano za kale zisizo na mashiko, na hivi sasa Wazayuni waliopora ardhi za Wapalestina na kuzibandika jina la Israel wanakabiliwa na majakamoyo mengi ya ufukara, ubaguzi, ukosefu mkubwa wa kazi, ufuska wa kijamii na kiserikali sambamba na udanganyifu wa wanasiasa unaopelekea serikali yoyote ya utawala wa Kizayuni isimalize muda wake madarakani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO