Tuesday, January 01, 2013

WAPALESTINA WAILALAMIKIA JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU

Wapalestina wamelalamikia kuendelea kimya cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika kuunga mkono haki zao na kutochukua hatua zozote za maana mkabala wa jinai zinazoongezeka kila uchao za Israel dhidi ya Wapalestina hasa wale wanaoshikiliwa mateka. Hii ni katika hali ambayo kusisitiza jumuiya hiyo kuendeleza siasa za mapatano na utawala wa Kizayuni kwa mujibu wa mpango wa amani unaoitwa Mpango wa Amani wa Kiarabu kumekosolewa kwa kiasi kikubwa na Wapalestina. Katika kulalamikia kimya cha jumuiya hiyo na misimamo yake ya kimaonyesho tu, siku ya Jumamosi Wapalestina waliandamana wakati Nabil al Arabi katibu Mkuu wa Jumuiya ya Arab League alipowasili katika makao makuu ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Waandamanaji hao sambamba na kusisitiza kwamba kadhia ya mateka wa Palestina wanaoshikiliwa na Israel haiwezi kutenganishwa na masuala ya Palestina, wamekosoa maafisa wa jumuiya hiyo kwa kutofanya jitihada zozote za kuachiliwa huru mateka hao kutoka katika makucha ya Israel. Siasa za kupatana na Israel na kunyamazia kimya jinai zake, hazijakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha siasa zake za kupenda kujitanua na kuzusha machafuko dhidi ya Wapalestina. Jinai za kutisha dhidi ya mateka wa Palestina na hatua ya hivi karibuni ya Israel ya kumkata vidole vya mkono mmoja wa mateka hao zinabainisha wazi matunda ya kuendeleza siasa za mapatano na utawala huo wa Kizayuni. Inaelezwa kuwa, vidole vya mikono vya Muhammad Ahmad Khalawi mateka wa Palestina vilikatwa hivi karibuni na askari wa Kizayuni, suala lililoakisiwa sana na vyombo vya habari lakini Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikalikalia kimya suala hilo. Matokeo mabaya ya mwenendo wa amani yanazidi kudhihirika siku baada ya siku katika maisha ya Wapalestina na hii ndio sababu fikra za walio wengi zikataka kuwekwa kando siasa hizo mapatano katika kukabiliana na Israel. Lakini jumuiya hiyo kwa kushinikizwa na nchi za Magharibi inasisitiza kuendelezwa mwenendo huo eti wa amani na Israel na hata inafanya jitihada za kuhuisha mpango uliofeli wa amani wa Kiarabu. Mpango huo ambao kwa mara ya kwanza ulipendekezwa na Saudi Arabia mwaka 2002, unajumuisha makubaliano ya amani ya pamoja ya nchi 22 za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutambuliwa rasmi utawala huo na nchi za Kiarabu, mkabala na kurejea nyuma Tel Aviv  kutoka katika mipaka ya kabla ya mwaka 1967. Mpango huo wa amani wa Kiarabu umepelekea kujisalimisha Waarabu kwa Israel na kukubali siasa zake za kibeberu. Kunyamaziwa kadhia ya wakimbizi na mateka wa Palestina katika mpango huo wa Kiarabu, ni sehemu ndogo tu ya udhaifu mkubwa unaoonyeshwa na serikali zenye kupatana na Israel kupitia mpango huo. Kupatana na Israel hakuna faida myingine yoyote ghairi ya kuufanya utawala huo uendelee kujitanua na kuzidisha kiburi chake cha kukanyaga kikamilifu haki za Wapalestina. Bila shaka sisitizo la watawala wa Kizayuni la kutotoa hata haki ndogo tu kwa Wapalestina linaakisi wazi matokeo mabaya ya mwenendo wa mapatano na Israel katika Mashariki ya Kati.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO