Zikiwa
zimesalia siku 10 tu kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais
Barack Obama wa Marekani, Waziri wa Kazi wa nchi hiyo ametangaza kujiuzulu.
Hilda Solis Mmarekani mwenye asili ya Uhispania alikuwa Waziri wa Kazi kwa
kipindi chote cha karibu miaka minne ya utawala wa Obama. Ijapokuwa Waziri wa
Kazi wa Marekani hana majukumu ya kuandaa shughuli za ajira nchini humo, hata
hivyo yeye pamoja na White House walikabiliwa na lawama na ukosoaji mkubwa kwa
kushindwa kupunguza kiwango cha watu wasiokuwa na ajira nchini humo. Wakati
Hilda Solis alipopewa jukumu la kuiongoza wizara hiyo, Wamarekani walitaraji
kuona ahadi iliyotolewa na Obama ya kuandaa nafasi milioni mbili na nusu za
ajira ikitekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu. Licha ya kupita miaka minne
nafasi hizo za ajira sio tu hazijapatikana bali idadi ya Wamarekani wasiokuwa
na kazi hivi sasa imefikia milioni nne. Hivi sasa kiwango cha watu wasio na
ajira nchini Marekani kinakaribia asilimia 7.8 ingawa inatarajiwa kuwa katika
miezi ijayo kiwango hicho kitashuka na kufikia asilimia saba. Hata hivyo, duru
zisizo rasmi zinaeleza kuwa, kiwango cha ukosefu wa ajira kinafikia mara mbili
ya kiwango kilichotangazwa na Wizara ya Kazi ya nchi hiyo. Hilda Solis
anahesabiwa kuwa waziri wa tano kujiuzulu tokea Rais Obama alipojipatia ushindi
kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba 6, 2012. Kabla ya hapo, Hillary
Clinton Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Timothy Geithner Waziri wa Fedha,
Leon Edward Panetta Waziri wa Ulinzi na Lisa Jackson Waziri wa
Hifadhi ya Mazingira walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao. Inatazamiwa
kuwa, baraza lijalo la mawaziri la Rais Obama litakuwa na mabadiliko ya
mlingano wa kiasili na kijinsia kulinganishwa na baraza la awamu ya kwanza.
Hivi sasa, mawaziri watatu wanawake waliokuwa kwenye baraza lililopita yaani
Hillary Clinton, Hilda Solis na Lisa Jackson wameshajing'atua na nafasi moja
kati ya hizo ya mambo ya nje imeshatangazwa kushikiliwa na mwanamume. Iwapo
Maseneta watashirikiana kumpitisha John Kerry kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za
Nje, shakhsia huyo ataliongoza jahazi la wanadiplomasia wa Kimarekani katika
kipindi cha miaka minne ijayo. Wamarekani waliokuwa na asili ya Kihispania
ambao walikuwa na ushawishi mkubwa katika ushindi wa Obama katika chaguzi za
miaka ya 2008 na 2012, hivi sasa wana wasiwasi baada ya kujiuzulu Hilda Solis,
kwani umepungua uwezekano wa kupewa tena nafasi za juu kwenye serikali ya
Obama. Wakati huohuo Obama amemuarifisha mshirika wake wa zamani katika Baraza
la Seneti Chuck Hagel, kuziba nafasi ya Leon Panetta kuiongoza Pentagon.
Ijapokuwa Hagen ni seneta aliyebobea kutoka mrengo wa Republican, amma
wanachama wenzake wa chama hicho walimtuhumu kwa kuyapuuza maslahi ya utawala
wa Kizayuni wa Israel na kwamba hakuonekana kuwa ngangari katika kukabiliana na
ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa minajili hiyo, Lobi zenye nguvu
za Kizayuni nchini Marekani ikiwemo Kamati ya Masuala ya Umma ya Marekani na
Israel AIPAC iliingilia kati na kuzuia Hagen kuchukua wadhifa nyeti wa
kuiongoza Wizara ya Ulinzi. Hali kadhalika, mrengo wa Republican unakosoa John
Owen Brennan kupewa jukumu la kuliongoza Shirika la Ujasusi la Marekani CIA.
Mrengo huo haukuridhishwa na utendaji wa serikali ya Obama katika kampeni za
kupambana na ugaidi akiwemo Brennan mwenyewe ambaye ni mshauri wa rais katika
operesheni dhidi ya vitendo vya kigaidi. Mrengo huo unataka Brennan asipewe
jukumu la kuiongoza CIA kwa vile alishindwa kuzuia shambulio la Ubalozi wa
Marekani huko Benghazi, Libya. Alaa kulli haal, kipindi cha kwanza cha miaka
minne cha uongozi wa Obama kimefikia ukingoni ambapo mpasuko wa kisiasa huko
Washington umezidi kuwa mkubwa mno katika hali ambayo katika miongo ya hivi
karibuni kumeshuhudiwa kila hatua inayochukuliwa na chama kimoja, hukabiliwa na
upinzani na radiamali kali kutoka chama kingine.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO