Monday, February 04, 2013

MAREKANI YAZIDISHA MASHAMBULIZI YA NDEGE ZISIZO NA MARUBANI NCHI KADHAA


Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta ameunga mkono hatua za Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na kusisitizia udharura wa kuendelezwa mashambulizi ya ndege za zisizo na rubani za shirika hilo nchini Pakistan na katika maeneo mengine ya duniani. Katika kuhalalisha hujuma hizo huko Pakistan, Panetta amedai kuwa, mashambulizi hayo yataendelea kwa ajili ya kuwaangamiza wanamgambo wa Al-Qaida nchini humo na katika maeneo mengine ya duania ili kwa njia hiyo Washington iweze kuzuia shambulizi la aina yoyote la magaidi dhidi ya Marekani. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, mashambulizi ya Marekani nchini Pakistan yanayofanyika kwa kisingizio cha kukabiliana na makundi ya kigaidi kama Al-Qaida na makundi mengine ya wabeba silaha yameua maelfu ya raia wasio na hatia yoyote. Suala hilo limezua upinzani mkubwa kutoka kwa serikali ya Pakistan na wananchi wa nchi hiyo dhidi ya Washington. Mashambulizi 362 ya ndege za Marekani zisizo na rubani yalifanyika nchini Pakistan tangu mwaka 2004, na 310 kati ya mashambulizi hayo yametekelezwa katika kipindi cha utawala wa Rais wa sasa wa Marekani Barack Obama. Mashambulizi hayo na ndege zisizo na rubani za Marekani yameuwa watu 3461 ambapo wengi wao ni raia wa kawaida.
Akijibu swali aliloulizwa kuhusiana na mashambulizi hayo yanayofanywa na CIA, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta amesema kuwa, mashambulizi hayo yaliyoanza baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 huko Marekani ni suala la dharura. Amesisitiza kuwa, mashambulizi hayo yataendelea kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokisema kuwa ni tishio kwa Washington. Kwa mujibu wa waziri huyo wa Marekani, mashambulizi hayo yanatakiwa kuendelezwa kwa njia za kisasa zinazoendana na kila zama.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta alikuwa msimamizi wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Pakistan na  mkuu wa Shirika la Ujasusi la CIA tangu mwaka 2009 hadi 2011. Hali hii inatilia mkazo kwamba, Rais Barack Obama anakusudia kushadidisha mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi katika kipindi cha pili cha utawala wake. Hatua hizo bila shaka zitaendelea kusababisha mauaji ya raia wa kawaida wa nchi ambazo zinalengwa na mashambulizi hayo, ikiwemo Pakistan, Afghanista, Yemen na Somalia.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani katika nchi mbalimbali duniani yanakosolewa mno na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu ambazo zinataka kuchukuliwe hatua madhubuti za kuisaili Washington na kuifikisha mbele ya vyombo vya sheria kutokana na idadi kubwa ya raia wa kawaida wanaouawa katika mashambulizi hayo.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO