Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe ametangaza kushiriki kwa mara ya sita kwenye uchaguzi wa rais utakaofanyika miezi michache ijayo nchini humo. Rais Mugabe ameyasema hayo jana wakati wa kuadhimisha kutimia miaka 89 ya kuzaliwa kwake, kwenye sherehe ndogo iliyofanyika nchini humo. Mugabe ambaye anaiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 33 sasa amepanga kufanya sherehe kubwa zaidi ya kuzaliwa kwake mwezi ujao itakayogharimu kiasi cha dola laki sita. Wakati Rais Mugabe akijiandaa kufanya sherehe mwezi ujao, hivi karibuni Tendai Biti Waziri wa Fedha wa nchi hiyo alitangaza kuwa, kuna kiasi cha chini ya dola 300 kwenye hazina ya serikali ya nchi hiyo. Zimbabwe licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi, inatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Rais Mugabe amesema kwenye hafla hiyo kuwa, mashinikizo ya Marekani na Uingereza yanafanyika kwa minajili ya kumuondoa yeye madarakani pamoja na chama chake cha Zanu PF. Duru ya tano ya uchaguzi wa rais nchini humo iligubikwa na ghasia na rangaito iliyopelekea chama cha Zanu PF na kile cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO