Marekani imeasisi kituo kipya cha ndege zake zisizo na rubani huko Niger kwa shabaha ya kupambana na wanagambo wa al Qaida na makundi yote yanayoliuga mkono kundi hilo barani Afrika na pia kwa lengo la kuviunga mkono vikosi vya Ufaransa katika vita vyao huko Mali. Gazeti za new York Times limeripoti kuwa Marekani imetuma huko Niger ndege zake zisizo na rubani aina ya Predator ili kuisaidia nchi hiyo katika kile ilichokitaja kuwa mapambano dhidi ya ugaidi. Ijumaa ya jana Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kuwa wanajeshi 100 wa nchi hiyo wametumwa nchini Niger ili kusaidia kukusanya taarifa za kiitelijenisia na kuwezesha usambazaji wa taarifa hizo kwa washirika wengine wa Marekani katika eneo na kwa vikosi vya Ufaransa vinavyoendesha oparesheni huko Mali. Afisa wa ulinzi wa Marekani ambaye hakutaja jina lake amesema kuwa ndege hizo za ujasusi hazijabeba silaha zozote na kwamba kazi yake ni kufanya ujasusi tu. Ndege hizo huenda zikatumika kuendeshea mashambulizi hapo baadaye iwapo itahitajika.
Viongozi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wametangaza kuwa nchi hiyo imetuma ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kuvisaidia vikosi vya Ufaransa vilivyoko huko Mali. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imedai kuwa imeazimia kutumia vituo vya ndege zisizo na rubani katika maeneo ya pwani na jangwani huko magharibi mwa bara la Afrika kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa harakati za wapinzani wa kisiasa katika nchi za eneo hilo.
Hadi sasa Washington imetumia ndege zake hizo zisizo na rubani katika baadhi ya nchi hususan huko Pakistan Afghanistan, Yemen na Somalia. Tangu baada ya tukio la Septemba 11 huko Marekani Pentagon imekuwa ikitumia ndege hizo kama silaha ya kufunika mashambulizi ya anga yanayofanywa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) katika pembe mbalimbali za dunia katika kile kinachotajwa kuwa ni mapambano dhidi ya ugaidi. Hata hivyo, viongozi wa Pentagon wanasisitiza kuwa ndege zisizo na rubani zilizotumwa huko Niger hazijabeba silaha wala makombora na kwamba zitatumika tu kwa ajili ya masuala ya ujasusi na kukusanya taarifa kuhusu wapinzani wa serikali ya Mali.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO