Saturday, February 23, 2013

OIC KUANZISHA TELEVISION YAKE


Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ina azma ya kutekeleza baadhi ya malengo likiwemo suala la kupambana na chuki na uadui dhidi ya Uislamu, kwa kuanzisha kanali yake ya televisheni. Taarifa zinasema kuwa, leo Jumamosi kinafanyika kikao cha wataalamu wa nchi wanachama wa OIC ambacho kitajadili kwa kina mikakati ya kuanzisha kanali ya televisheni itakayorusha matangazo yake kwa lugha za Kiarabu, Kiingereza na Kifaransa. Esam al Shanti Mkurugenzi wa Idara ya Habari wa OIC amesema kuwa, lengo kuu la kuanzishwa kwa kanali hiyo ya televisheni ni kuonyesha sura halisi ya Kiislamu, kukabiliana na vitendo vya kuufanya Uislamu uogopwe na hasa katika nchi za Magharibi na hali kadhalika kukurubisha staarabu za Mashariki na Magharibi na Kaskazini na Kusini. Hakuna shaka kuwa, vyombo vya kupasha habari vina nafasi kubwa ya kuathiri matukio ya kimataifa na fikra za walio wengi duniani na hasa katika zama hizi za utandawazi. Hali kadhalika, vyombo vya kupasha habari licha ya kuwa na athari kubwa katika kusambaza tamaduni mbalimbali, vinahesabiwa pia kuwa wenzo wa kutoa huduma kwa madola ya Kimaghairbi. Aidha kuna baadhi ya vyombo vya habari katika ulimwengu wa Kiislamu ambavyo havijishughulishi na kukabiliana na vitendo vya kiadui dhidi ya Uislamu, bali vimekuwa bega kwa bega na vyombo vya Magharibi katika kuleta mifarakano ya kimadhehebu na kuzipaka matope baadhi ya nchi za Kiislamu. Nafasi hizo za uharibifu na utibuaji wa vyombo vya habari vya Kimagharibi na vya Kiarabu zimefichuka zaidi katika kipindi cha miaka miwili  iliyopita, ambapo ulimwengu umeshuhudia mwamko na Kiislamu na wimbi kubwa la wananchi wa nchi za Kiarabu lililokuwa dhidi ya watawala vibaraka. Kuhusu suala hilo, OIC ikiwa ni miongoni mwa jumuiya kubwa ulimwenguni, haikuwa na athari yoyote muhimu katika matukio yaliyojiri miaka miwili iliyopita na wala kuweza kutoa ushawishi wake katika kukabiliana na vyombo vya habari vya Magharibi na vile vya nchi za Kiarabu vinavyochochea  mifarakano ya Kimadhehebu. Hakuna shaka kuwa, kwa kuzingatia mazingira ya kiadui yaliyoko dhidi ya Uislamu ulimwenguni na hali kadhalika fitina za kimadhehebu zilizoko katika eneo, huu ni wakati mwafaka kwa jumuiya ya OIC kuchukua maamuzi hayo mazito na muhimu ya kuanzisha kanali ya televisheni ambayo itaweza kubadilisha anga ya kiadui iliyotanda dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Alaa kulli haal, baada ya kuanzishwa kanali hiyo ya televisheni ya OIC, suala muhimu ni kuwa,  chombo hicho hakipasi kuathiriwa  kiutendaji na watawala wa baadhi ya nchi za Kiarabu, kwani utendaji wake unapasa kuwa na maslahi kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu kwa kuondoa hitilafu zilizopo. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC iliundwa tarehe 25 Disemba mwaka 1969 na hivi sasa ina jumla ya wanachama 57.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO