Friday, March 08, 2013

KOREA KASKAZINI YATISHIA KUISHAMBULIA MAREKANI KWA NYUKLIA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema nchi hiyo imejiondoa kwenye mkataba wa 1953 wa usitishaji vita na jirani yake Korea Kusini na kutishia kuishambulia Marekani kwa kombora la nyuklia. Afisa huyo wa ngazi za juu wa Korea Kaskazini amesema Marekani inatumia kisingizio cha mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini kama wenzo wa kuishambulia kijeshi Pyongyang. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini pia amesema ifikapo Machi 11 iwapo Washington na Seoul hazitasitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika Peninsula ya Korea, Pyongyang haitakuwa na jingine bali kuchukua hatua za kijeshi kulinda maslahi yake. Hata hivyo baadhi ya duru zinasema vitisho vya Korea Kaskazini havina mashiko kwani licha ya kuwa na silaha za nyuklia, nchi hiyo haina uwezo wa kuunda mitambo ya kurushia makombora hayo hadi Marekani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO