Sunday, March 10, 2013

MAHARAMIA WAIACHIA MELI WALIYOITEKA


Maharamia wa Kisomali wameiachia huru meli ya shehena ya kemikali waliyoiteka nyara tangu mwaka mmoja uliopita ikiwa na mabaharia 20 baada ya kupokea kikomboleo. Hayo yameelezwa na maharamia wenyewe pamoja na waziri wa serikali inayojiendeshea mambo yake ya Puntland. Maharamia hao wamesema wameiachilia huru meli hiyo inayomilikiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu Imarati ambayo waliiteka nyara mwezi Machi mwaka uliopita katika bahari ya Oman. Said Mohammed Rage, Waziri wa Bandari na Kupambana na Uharamia wa serikali ya eneo la Puntland lililoko kaskazini mashariki mwa Somalia amethibitisha kutolewa kwa kikomboleo cha fedha kwa ajili ya kuachiwa huru meli hiyo ya Imarati. Ingawa haikufahamika ni aina gani ya shehena iliyokuwemo ndani ya meli hiyo au nani waliotoa kikomboleo cha kuachiwa kwake lakini kwa kawaida wamiliki wa meli na wa shehena iliyobeba huwa ndio wanaotoa malipo ya kikomboleo kupitia kanuni za bima. Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita wa Februari, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alitoa msamaha kwa mamia ya maharamia vijana ili kujaribu kuwatoa kwenye magenge ya kiharamia yanayohusika na utekaji nyara meli na  kwa lengo la kupunguza tishio dhidi ya safari za meli katika pwani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika…/

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO