Sunday, March 24, 2013

MBUNGE WA UINGEREZA AKOSOA VYOMBO VYA HABARI VYA MAGHARIBI


George Galloway, Mbunge wa Uingereza amevikosoa vyombo vya habari vya Magharibi na kusisitiza kwamba, vinafanya makusudi kutoripoti inavyotakiwa kuhusiana na mgomo wa kutokula chakula wa wafungwa wa gereza la Guantanamo Bay. Galloway amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya Kimataifa ya Russia Today na kusisitiza kwamba, lau kama yale yanayotokea katika gereza la Guantanamo Bay yangelikuwa yametokea sehemu nyingine basi vyombo vya habari vya Magharibi vingekuwa vikipigana vikumbo katika kuripoti matukio ya tukio hilo. Mbunge huyo mashuhuri wa Uingereza amesema kuwa, mashirika ya kijasusi ya Uingereza ya M15 na M16 yanashirikiana na viongozi wa Marekani katika baadhi ya mambo na ameitaka serikali ya London kufanya kila iwezalo ili kuachiliwa huru Shaker Aamer mfungwa pekee wa Uingereza aliyesalia katika gereza la Guantanamo. Mgomo wa kula chakula unaoendelea kufanywa na wafungwa walioko katika jela ya Guantanamo umeingia katika wiki yake ya saba huku wataalamu wa kitiba na mawakili wanaowatetea wafungwa hao wakionya kuhusu kudhoofika kiafya wafungwa waliogoma kula chakula.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO