Thursday, March 07, 2013

MWAKILISHI WA IRAN AANDIKA BARUA KADHAA KWA MKUU WA IAEA

Ali Asghar Sultaniyeh, Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amemwandikia barua tatu Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo kumtaka awajibike mbele ya Bodi ya Magavana wa IAEA kuhusiana na maudhui tatu muhimu.
Katika barua hizo tatu alizoziwasilisha hapo jana Sultaniyeh amesisitiza juu ya ulazima wa kutunzwa taarifa za siri katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na kulalamikia mwenendo wa baadhi ya nchi za Ulaya wa kutotekeleza wajibu wao kwa IAEA kutokana na kuendelea kuwekwa silaha za nyuklia katika nchi hizo. Aidha amekosoa mwenendo wa Marekani wa kuendelea kukiuka mkataba wa kuzuia uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT kwa kuendelea kuunda na kueneza silaha hizo hatari katika baadhi ya nchi za Ulaya. Mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Atomiki amelalamikia pia utendaji wa Amano kuhusiana na utekelezaji majukumu ya ukaguzi na kuwasilisha matokeo ya ukaguzi huo kwa Bodi ya Magavana wa IAEA.
Katika barua yake ya kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Ali Asghar Sultaniyeh amezungumzia Protokali ya Nyongeza ya wakala huo na kumweleza Amano kwamba, kisheria, hati hiyo haina ulazima wa utekelezaji bali ni suala la hiyari kwa nchi wanachama wa IAEA, na kwa sababu hiyo nchi nyingi wanachama ikiwemo Iran zinatekeleza Protokali ya Nyongeza kwa sura ya hiyari na kujitolea. Barua hiyo ya kwanza imesisitiza kuwa katika hatua ya kujenga imani na moyo wa kuaminiana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilijitolea kuitekeleza kwa hiyari Protokali ya Nyongeza, lakini kwa kuzingatia uhuru wake wa kitaifa na mamlaka ya kujitawala bado haijaipasisha rasmi itifaki hiyo na kwa msingi huo hakuna ulazima wa kisheria kwake wa kuitekeleza. Barua hiyo aidha imekumbusha kuwa licha ya ushirikiano huo ulioonyeshwa na Iran katika kipindi cha kati ya mwaka 2003 hadi 2006, kwa masikitiko ni kwamba katika kipindi hicho hicho na kwa mashinikizo ya baadhi ya nchi za Magharibi na kwa utashi wa kisiasa, Bodi ya Magavana wa IAEA ilipasisha maazimio saba yasiyo ya kisheria dhidi ya Iran, hatua iliyodhihirisha wazi kwamba faili la nyuklia la Tehran halishughulikiwi kiufundi wala kisheria bali ni kwa sababu na malengo ya kisiasa tu.
Barua ya pili ya mwakilishi wa Iran katika IAEA kwa Mkurugenzi Mkuu wa wala huo imeeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kwa muda mrefu sasa taarifa za siri zinazowasilishwa na Iran kwa Wakala wa Atomiki zimekuwa zikivujishwa na kutoka nje ya taasisi hiyo ya kimataifa. Sultaniyeh amefafanua kuwa mwenendo huo wa kuvujishwa taarifa za siri zinazowasilishwa kwa IAEA umekuwa jambo la kawaida na kwamba licha ya Iran kulalamikia hali hiyo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haujachukua hatua yoyote ya maana juu ya suala hilo.
Katika barua yake ya tatu kwa Yukiya Amano, mwakilishi wa Iran katika IAEA ameashiria mwenendo wa Marekani na nchi za Ulaya wa kutowajibika na kutekeleza wajibu na majukumu yao kisheria kutokana na kuendelea kumiliki silaha za nyuklia na kusisitiza kwamba nchi hizo haziuheshimu na kuutekeleza mkataba wa NPT. Sultaniyeh amesema Mkurugenzi Mkuu wa IAEA anatakiwa aliripoti suala hilo na ambalo linapasa kuchukuliwa hatua ya haraka na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO