Serikali ya Ufaransa imekumbwa na kizungumkuti iwapo itoe silaha kwa waasi nchini Syria au la na badala yake wanaendelea kusubiri maamuzi ya Umoja wa Ulaya EU ambao utaamua juu ya ombi lao na Uingereza kutaka kuondoa kizuizu cha kupeleka silaha Damascus. Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameweka bayana kwa sasa hawana uhakika kama wataweza kuwasaidia Waasi wanaopambana na serikali ya Rais Bashar Al Assad kwa kuwapatia silaha ili waendelea na vita vyao. Hollande amesema kwa sasa hilo limebaki kuwa chini ya Umoja wa Ulaya EU licha ya Ufaransa na Uingereza kuwa tayari hapo kabla kuwasaidia waasi kwa kuwapatia silaha.Katika hatua nyingine rais Bashar al-Asad amelaani vikali shambulio la roketi lililotekelezwa kulenga wanafunzi wa chuo kikuu cha mjini Damascus, shambulio ambalo rais Asad amewatuhumu upinzani. Kwenye taarifa yake rais Asad amesema kuwa shambulio hilo linaendelea kudhihirisha ukatili ambao umekuwa ukifanywa na waasi wa Syria dhidi ya wananchi wasio na hatia na kwamba makundi ya kigaidi yameendelea kuwasaidia waasi kutekeleza mashambulizi zaidi dhidi ya Serikali na watu wake. Hata hivyo upande wa waasi umekanusha kutekeleza shambulio hilo ambalo lilishuhudia wanafunzi kumi na mbili wakipoteza maisha kwenye mgahawa wa chuo ambako walikuwa wakinywa chai kabla ya kuvurumishwa kwa roketi hiyo.Halikadhalika nchi za Iran, Korea Kaskazini na Syria zimepinga kutiwa saini mkataba maalumu wa kutazama biashra ya silaha duniani, mkataba ambao ulikuwa unahitaji baraka za nchi wanachama 193 ili uweze kufanya kazi. Balozi wa Australia Peter Woolcott amesema kuwa mkutano huo umeshindwa kutoka na maamuzi baada ya nchi hizo tatu kukataa kuunga mkono azimio hilo ambalo lililenga kuwepo uangalizi wa karibu wakati nchi zinapokuwa zinanunua silaha kwa matumizi ya kiusalama. Awali balozi huyo alilazimika kuahirisha kikao baada ya nchi za Iran, Korea Kaskazini na Syria kukataa kuendelea kujumuika kwenye mkutano huo ka madai kuwa baadhi ya mataifa yamekuwa yakiwaongelea vibaya kuhusu matumizi ya silaha ambazo nchi hizo imekuwa ikinunua.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO