Friday, March 08, 2013

UFARANSA YAJIANDAA KUONDOA WANAJESHI WAKE MWEZI UJAO


Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema kuwa nchi yake itaanza kuondoa wanajeshi wake kutoka Mali mwezi Ujao. Aliongeza kuwa harakati za mwisho za jeshi dhidi ya wapiganaji wa Mali zitaendelea hadi mwishoni mwa Machi kufikia Aprili. Bwana Hollande alisema kuwa harakati hizo zilipelekea kuuawa kwa viongozi wa wapiganaji, ingawa hakuwataja majina.

Mwanajeshi mmoja wa Ufaransa aliuawa pamoja na wapiganaji 10 wakati wa makabiliano kati yao, kilomita miamoja Mashariki mwa mji wa Gao. Bwana Hollande alisema kuwa viongozi wa wapiganaji wameangamizwa ingawa haijulikani ikiwa anazungumzia viongozi wawili waliouawa wiki jana. Nchi ya Chad, imesema kuwa wanajeshi wake, waliokuwa wanasaidiana na wanajeshi wa Ufaransa, waliwaua makamanda wawili wakuu wa wapiganaji,Abdelhamid Abou Zeid kutoka kundi la al-Qaeda na kiongozi mkongwe wa wapiganaji wa kiisilamu Mokhtar Belmokhtar.
Wanajeshi wa Ufaransa hata hivyo bado hawajathibitisha taarifa hizo. Takriban wanajeshi 4,000 wangali wako nchini Mali. Wanajeshi wa Mali kwa ushirikiano na wanajeshi wengine kutoka katika nchi kadhaa za Afrika, ikiwemo wanajeshi elfu mbili kutoka Chad wamehusika na harakati hizo. Ufaransa awali ilisema kuwa idadi ya wanajeshi itaanza kupungua kuanzia mwezi Machi ikiwa mipango yote ingekwenda kama ilivyopangwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO