Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uviondoe vitongoji vyote ulivyojenga katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan wa ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Kikao cha baraza hilo kilichofanyika siku ya Ijumaa, aidha kimeutaka utawala haramu wa Kizayuni ulipe fidia kwa hasara ulizowasababishia Wapalestina kutokana na ujenzi wa vitongoji hivyo. Kati ya nchi zote 47 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni Marekani pekee ndiyo iliyopinga uamuzi huo uliopitishwa na baraza hilo juu ya ulazima wa kuondolewa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.
Marekani imeweka pingamizi ya kuzuia kulaaniwa utawala wa Kizayuni katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika hali ambayo katika safari yake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Rais wa Marekani Barack Obama alijidai kutoa matamshi ya kimaonyesho ya kukosoa ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Wapalestina. Migongano ya maneno na vitendo katika misimamo ya Marekani inadhihirisha jinsi nchi hiyo inavyozidi kutumia mbinu za hila na hadaa ili kuficha ukweli kwamba inaunga mkono kikamilifu siasa za kujipanua za utawala haramu wa Kizayuni. Inafaa kuashiria hapa kwamba wakati wa safari ya hivi majuzi ya Obama huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu viongozi wa utawala wa Kizayuni walitangaza kuwa awamu mpya ya ujenzi wa vitongoji itaanza hivi karibuni. Yair Lapid, waziri mpya wa fedha wa utawala haramu wa Israel alitangaza siku ya Ijumaa kwamba utawala huo umeshapasisha mpango mpya wa kujenga maelfu ya nyumba katika maeneo ya Ufukwe wa Magharibi na Baitul Muqaddas. Lengo la utawala wa Kizayuni la kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ufukwe wa Magharibi unaoukalia kwa mabavu ni kulidhibiti kikamilifu eneo hilo na kuliunganisha na ardhi za Palestina zilizovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel. Alaa kulli hal, kushadidi siasa za kujipanua za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Paletsina na hatua za Marekani za kupinga na kuzuia kulaaniwa kwa namna yoyote ile utawala huo ghasibu katika taasisi za kimataifa ni ithbati tosha kuwa Washington inatoa baraka kamili kwa Israel za kuendeleza siasa zake hizo katika Palestina unayoikalia kwa mabavu. Masuala hayo yanadhihirisha matokeo hasi ya safari ya Obama katika Mashariki ya Kati na vilevile kubainisha ukweli kwamba harakati mpya za Marekani katika eneo hili zinazotekelezwa katika kalibu ya kufufua mchakato wa mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel hazina lengo jengine ghairi ya kuzidi kuzipigisha mnada haki za Wapalestina, kuuzatiti na kuupa nguvu zaidi uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa utawala wa Kizayuni na kuhalalisha sera za utawala huo ghasibu za kuzidi kujipanua katika ardhi za Palestina…
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO