Wednesday, March 13, 2013

WAASI WA PKK WAWAACHIA HURU MATEKA


Waasi wa jamii ya Kikurdi, Kurdistan Workers Party (PKK) wamewaachia huru mateka nane wa Uturuki ikiwa ni mwitikio wa mpango mpya wa amani wa Ankara unaolenga kumaliza mgogoro wa miaka 29 katika eneo la kusini mashariki mwa nchi ya Uturuki. Kuachiliwa kwa mateka hao waliokuwa wakishikiliwa kwa miaka miwili kaskazini mwa Iraq kunakuja baada ya kiongozi wa PKK aliye kifungoni Abdullah Ocalan kusema ana matumaini ya kuona wafungwa wanakuwa na familia zao. Kiongozi wa ulinzi wa PKK Bawer Pirson, amewaambia waandishi wa habari kuwa wameitikia wito wa kiongozi wao na kuamua kuwaachia wafungwa hao nane na wanatarajia jitihada zao zitafanikiwa katika mchakato wa kusaka amani. Aidha, kiongozi huyo amesema wanatarajia Uturuki pia itamuachia kiongozi wao Abdullah Ocalan kwani bila kufanya hivyo mchakato wa amani kati yao hautafanikiwa. Pirson amesema wanaiachia uamuzi mahakama ya Uturuki kuhakikisha inaendeleza nia yao njema ya kutafuta amani.
PKK inataka kuachiliwa kwa mamia kwa maelfu ya wanasiasa na wanaharakati wake waliowekwa kizuizini kwa makosa ya kujihusisha chama cha waasi cha PKK. Pande zote zilizopo katika mgogoro huo zimetoa masharti ambayo kila mmoja anaona yatakuwa na hatma nzuri katika mpango wa amani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO