Saturday, March 23, 2013

WALIOTAKA KUMPINDUA KABILA WAKAMATWA

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwatia mbaroni washukiwa wawili waliokuwa wakipanga njama za kutaka kumpindua Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo. Richard Muyej Mangez Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewaambia waandishi wa habari kwamba mmoja kati ya wapanga njama hizo ni Dakta Jean Pierre Kanku Mukendi raia wa Ubelgiji  na Isidore Madimba Mungombe Kamanda wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini Kongo. Amesema kuwa, raia huyo wa Ubeljgiji amefanya vikao kadhaa na raia wa Kongo walioko Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani kwa lengo la kumuondoa kwa nguvu Rais Kabila madarakani. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kongo ameongeza kuwa, jeshi la polis limekamata bunduki tano, kombora na silaha nyingine kadhaa ndani ya hoteli aliyofikia mshukiwa huyo. Waziri Richard Muyej Mangez wa Kongo amesema kuwa, watu hao watafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya ujasusi, njama za kutaka kumuua Rais Kabila, kula njama na kuipindua serikali ya Kinshasa na  kupatikana na silaha kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO