Miji ya Cairo na Alexandria jana ilikuwa uwanja wa mapigano na maandamano ya waungaji mkono na wapinzani wa serikali ya sasa ya Cairo. Mjini Cairo maandamano na mapigano ya pande hizo mbili yalisimamisha shughuli za biashara katika maeneo ya kandokando ya Medani ya Tahrir na kuwalazimisha wafanya biashara kutumia bunduki za kuwindia wanyama wakiwalenga waandamanaji. Watu kumi wamejeruhiwa katika mapigano hayo. Muungano wa wapinzani wa serikali ya Rais Muhammad Mursi hususan Harakati ya Uokovu wa Kitaifa ulikuwa umewataka wafuasi wake kushiriki kwa wingi katika maandamano hayo.
Mji wa Alexandria pia ulikumbwa na hali kama ile ya Cairo. Wafuasi wa kambi mbili za waungaji mkono na wapinzani wa serikali walitwangana na kushambuliana kwa kutumia silaha za aina mbalimbali. Kanali ya televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon pia imeripoti kuwa mapigano ya silaha yameshuhudiwa mbele ya ofisi ya Harakati ya Ikhwanul Muslimin mjini humo.
Mapigano hayo yalianza wakati wa wafuasi wa kambi ya upinzani dhidi ya serikali ya Cairo walipotaka kuvamia ofisi za Harakati ya Ikhwanul Muslimin. Mapigano hayo yalishadidi zaidi baada ya wapinzani kuanza kutoa nara dhidi ya serikali ya Rais Muhammar Mursi na kusababisha ghasia kubwa katika mji mzima wa Alexandria.
Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, machafuko ya sasa ya Misri yanahusiana na tukio la kuuzuliwa Mwendesha Mashtaka Mkuu Abdul Majiid Mahmoud. Mwezi Novemba mwaka jana Rais Mursi alimfuta kazi Abdul Majiid ambaye aliamua kufungua kesi mahakamani dhidi ya uamuzi huo. Baada ya kusikiliza kesi hiyo Mahakama ya Rufaa ya Misri ilimwamuru Rais wa nchi hiyo kufuta uamuzi wake na kumrejesha kazini Mwendesha Mashtaka Mkuu. Uamuzi huo umepongezwa na mrengo wa kiliberali nchini Misri ambao umeutaja kuwa ni ushindi wa utawala wa sheria na ishara ya uhuru wa mahakama za nchi hiyo. Hata hivyo duru za kieneo zinasema kuwa kufutwa uamuzi wa Rais wa Misri ulikuwa mwanzo wa mpambano mkali baina ya serikali ya Cairo na taasisi ya mahakama. Suala hilo hususan katika mazingira yanayotawala sasa nchini Misri, ni tishio kubwa kwa mapinduzi ya wananchi. Vilevile Waziri Mkuu wa Misri Hesham Qandil amesema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa na kusema kuwa moja ya matatizo hayo ni ghasia na ukosefu wa amani.
Hali hiyo ya ukosefu wa amani imetumiwa vibaya na baadhi ya makundi yasiyokuwa na utambulisho wa kisiasa na kumlazimisha Rais Mursi kutahadharisha kwamba baadhi ya mirengo ya kisiasa na hata wanasiasa wa Misri wanatumia vyombo vya habari kuchochea wananchi. Mursi amesema kuna tofauti kubwa baina ya haki ya wananchi ya kufanya maandamano ya amani ya kudai haki zao na machafuko na ghasia zinazoharibu mali ya umma. Rais wa Misri amevitaka vyombo vya usalama kukabiliana na machafuko hayo.
Ghasia za sasa za Misri zimetoa dharba kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo. takwimu zinaonesha kuwa, machafuko ya kisiasa na ghasia za Misri zimeisababishia nchi hiyo hususan sekta ya utalii hasara ya dola bilioni moja. Wachambuzi wa mambo wanasema hasara hiyo huenda ikaongezeka zaidi iwapo serikali ya Cairo itashindwa kudhibiti ghasia na machafuko yanayotatiza shughuli za utalii.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO