Serikali iliyochaguliwa na wananchi ya Palestina chini ya uongozi wa Ismail Hania imelaani matamshi yaliyotolewa na Rais Barack Obama wa Marekani katika safari yake ya sasa huko Israel. Barack Obama alisema jana baada ya kuwasili ardhi zinazokaliwa kwa mabavu huko Israel kwamba Marekani inafungamana kikamifu na kulinda usalama wa utawala wa Kizayuni Israel kwa sababu usalama wa Israel ni sawa na usalama wa Marekani.
Obama ambaye alikuwa akizungumza na waandishi habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa, usalama wa Israel una umuhimu mkubwa kwa Marekani na unapaswa kulindwa. Amesisitiza pia juu ya kudumishwa misaada ya fedha na silaha ya Washington kwa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa ahadi ya Marekani ya kulinda usalama wa Israel haina mjadala. Hapana shaka kuwa sisitizo la viongozi wote wa Marekani juu ya kudumishwa misaada na himaya ya pande zote ya Washington kwa utawala ghasibu wa Israel inadhihirisha sera za siasa za nje za Marekani na kiwango cha udhalili wa viongozi hao mbele ya Wazayuni.
Tukirejea kwenye safari ya sasa ya Rais Barack Obama, ni wazi kuwa malengo ya safari hii ni kupanua zaidi uhusiano wa Washington na Tel Aviv na kupanga mikakati zaidi ya kuendeleza njama dhidi ya mataifa ya Mashariki ya Kati. Katika fremu hiyo, Obama amefanya safari yake ya sasa huko Israel huku eneo la Mashariki ya Kati likiwa bado linaathiriwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kushadidi harakati za wananchi dhidi ya tawala vibaraka, tegemezi kwa Magharibi na zenye uhusiano na Israel. Hali hiyo imevuruga mlingano uliokuwepo katika eneo la Mashariki ya Kati, suala ambalo linawatia kiwewe viongozi wa Marekani na Israel. Kwa msingi huo viongozi hao wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa shabaha ya kupanga njama na mikakati ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya watu wa mataifa ya eneo hili. Rais Barack Obama wa Marekani amewasili huko Israel wakati dola hilo bandia likiendelea kutoa vitisho vya vita na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mataifa ya Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo baadhi ya weledi wa mambo wanasema kuwa safari hiyo ni sawa na ruhusa na uungaji mkono wa serikali ya Washington kwa utawala wa Kizayuni na jinai zake katika eneo hili.
Ukweli ni kuwa himaya na misaada ya Marekani kwa utawala katili wa Israel inagusa sehemu pana zaidi hususan masuala ya kiuchumi na kijeshi na huipa Israel msaada wa dola bilioni tatu na sehemu kubwa ya fedha hizo hutolewa katika sura ya silaha na zana za kivita. Kiwango kikubwa cha misaada ya nchi za Magharini kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kinaweka wazi mipango maalumu ya pande hizo ya kudumisha jinai na uhalifu wa utawala huo haramu katika eneo la Mashariki ya Kati. Takwimu zinaonesha kuwa ushirikiano wa Marekani na Israel umeongezeka zaidi katika kipindi cha utawala wa Rais Barack Obama. Misaada ya pande zote ya Marekani kwa utawala huo wa Kizayuni wakati wa mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ni kielelezo halisi cha uhusiano wa Obama na Wazayuni. Matunda ya kujikomba Barack Obama kwa Wazayuni yalionekana katika misaada ya lobi za makundi ya Wazayuni katika uchaguzi wa Rais wa Marekani ambayo ilimsaidia kushinda tena kiti cha rais. Uungaji mkono wa Marekani na Rais Barack Obama kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za Israel umepingwa vikali na kulaaniwa na wananchi wa Palestina.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO