Sunday, March 24, 2013

WAZIRI MKUU WA LEBANON AJIUZULU


Ripoti kutoka Lebanon zinaeleza kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Miqati amejiuzulu wadhifa wake huo. Kujiuzulu kwa Miqati kumejiri katika hali ambayo mnamo wiki za hivi karibuni Lebanon imeghariki kwenye dimbwi la mgogoro wa kisiasa kutokana na kuongezeka hitilafu baina ya vyama na mirengo ya kisiasa hususan juu ya namna ya kufanyika uchaguzi wa bunge la nchi hiyo. Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Lebanon kunaonyesha kuwa nchi hiyo imeingia kwenye mkwamo wa kisiasa, hali inayodhihirisha jinsi mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo unavyozidi kuwa tata. Joto la mgogoro huo linaendelea kutokota katika hali ambayo kushtadi kwa vitendo vya machafuko na vya kuchochea mivutano vinavyofanywa na makundi ya kisalafi huko Tripoli kaskazini mwa Lebanon na vile vile mivutano ya kimatapo katika baadhi ya maeneo vimeitumbukiza nchi hiyo kwenye hali ya mchafukoge na ukosefu wa usalama kwa miezi kadhaa sasa. Kama vile haitoshi katika miezi ya hivi karibuni Lebanon imegeuzwa pia kuwa uwanja wa harakati za makundi ya kigaidi ya Syria na waungaji mkono wao zenye lengo la kuupanua mgogoro wa nchi hiyo hadi ndani ya ardhi ya Lebanon na kuvuruga amani na uthabiti nchini humo.
Waziri Mkuu wa Lebanon amejiuzulu baada ya Baraza la Mawaziri la nchi hiyo likiongozwa na Rais Michel Suleiman kupinga mapendekezo yaliyotolewa na Miqati. Akitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu hapo jana usiku, Najib Miqati alisema sababu kuu iliyomfanya achukue uamuzi huo ni kutopitishwa mapendekezo yake katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika mapema jana. Mapendekezo hayo ya Waziri Mkuu wa Lebanon ni kutaka kurefushwa kipindi cha uongozi wa Meja Jenerali Ashraf Rifi, kamanda mkuu wa vikosi vya usalama wa ndani na vilevile kuundwa tume ya usimamizi wa uchaguzi wa bunge pendekezo ambalo lilipingwa na akthari ya mawaziri kutokana na kukinzana na sheria za nchi. Kwa mtazamo wa duru za habari za Lebanon mashinikizo ya mrengo wa Machi 14 unaoundwa na makundi yenye mielekeo ya Kimagharibi ndiyo yaliyomsukuma Miqati na kumfanya awasilishe mapendekezo hayo.Rais Michel Suleiman ameukubali uamuzi wa kujiuzulu Waziri Mkuu Miqati na kuitaka serikali iliyopo iendelee kufanya kazi kwa muda sambamba na kuwataka wabunge waanze kufanya mashauriano ya kumpendekeza na kumuarifisha Waziri Mkuu mpya kwa ajili ya kuunda serikali. Kwa kuzingatia matukio yanayojiri nchini Lebanon wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo wametoa mapendekezo mbalimbali kuhusiana na muundo wa serikali ijayo ili kuiwezesha nchi hiyo kuvuka salama dhoruba ya mgogoro wa kisiasa uliopo yakiwemo ya kuundwa serikali ya uokovu wa kitaifa au serikali ya umoja wa kitaifa…/

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO