Wednesday, April 10, 2013

WAPALESTINA WALALAMIKIA SERIKALI YAO KUFANYA MAZUNGUMZO NA ISRAEL

Wapalestina wanaendelea kulalamikia siasa za Mamlaka ya Ndani ya Palestina za kufanya mapatano na Israel, na ushiriki wake katika duru mpya ya harakati zinazofanywa kwa hila na Marekani za kuhuisha mwenendo wa upatanishi, ili kuwapokonya zaidi fursa Wapalestina. Kuhusu hilo naibu wa kwanza wa spika wa bunge la Palestina ameitaka harakati ya Fat-h kuhitimisha mazungumo ya amani na aduia Mzayuni na kushikamama na chaguo la kistratejia la muqawama. Hayo yanajiri huku harakati ya Jihadul Islami ya Palestina pia ikisisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Harakati hizo za Washington zenye lengo la kuhuisha mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati zilizoshika kasi sambamba na safari ya John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani huko Israel, zimewafanya walimwengu watambue zaidi ukubwa wa njama za pamoja za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Katika fremu hiyo, John Kerry ametaka kuanza mazungumzo eti ya kusaka amani bila masharti yoyote. Sisitizo la Kerry la kutotolewa masharti yoyote ya utangulizi kabla ya mazungumzo hayo kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Israel, limelenga sharti lililotolewa na mamlaka hiyo la kutoendelea mazugumzo hadi pale Israel itakaposimamisha ujenzi wa vitongoji vyake vya walowezi katika maeneo ya Wapalestina. Utendaji wa watawala wa Marekani katika mazungumzo hayo eti ya kusaka amani ya Mashariki ya Kati ni wa kiupendeleo kiasi kwamba, hawako tayari kuzingatia hata matakwa madogo ya Wapalestina, na mkabala wake wanaendelea kusisitiza kwamba Mamlaka ya Ndani iendelee kuipatia fursa zaidi Israel, suala ambalo linashuhudiwa katika kila duru ya mazungumzo hayo. Mamlaka ya Ndani ya Palestina inashiriki katika harakati hizo za kinafiki za Marekani za kuhuisha mwenendo huo wa upatanishi katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni Israel sio tu haijapunguza vitendo vyake vya kutumia mabavu dhidi ya Wapalestina bali pia imezidisha hatua zake za kikatili na za kupenda kujitanua dhidi ya taifa la Palestina. Inaonekana kuwa, utawala huo ghasibu unatumia fursa ya makubaliano ya amani na usitishaji vita ili kufanya jinai zaidi dhidi ya Wapalestina. Marekani inadai kuwapatanisha bila upendeleo Wapalestina na Israel, huku daima ikiuhami zaidi utawala wa Kizayuni kisiasa, kiuchumi na kijeshi, suala linaloonyesha wazi jinsi madai hayo ya Marekani yasivyo ya kweli. Hii ndiyo sababu Wapalestina wanasisitiza kuwa, hawapaswi kuwa na matumaini na mazungumzo hayo kwa kuwa hayana lengo lingine isipokuwa kuuimarisha zaidi utawala huo na kuwapokonya kikamilifu Wapalestina haki zao. Kwa msingi huo, Wapalestina wengi wanasisitiza kutofanya suluhu na utawala wa Kizayuni na kuendelea kusimama kidete dhidi ya utawala huo ghasibu unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu. Hasa kwa kuzingatia kuwa, muqawama umewapatia wananchi wa Palestina mafanikio mengi. Miongoni mwayo ni kuondoka kwa madhila Israel huko Gaza mwaka 2005 na kushindwa utawala huo katika vita wiwili dhidi ya Gaza yaani vita vya siku 22 mwaka 2009 na vita vya siku 8 mwaka uliopita wa 2012. Mafanikio hayo tuliyoyataja yanabainisha kuwa, njia pekee ya kufikiwa matakwa muhimu ya Palestina ni kuendelezwa Intifadha suala ambalo linatiliwa mkazo na wananchi, shakhsia na makundi yote ya mapambano ya Palestina.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO