Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amesema nchi yake itajibu haraka chokochoko zozote kutoka nchi jirani ya Korea Kaskazini na kuitaka Wizara ya Ulinzi kukaa ange huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda katika Peninsula ya Korea. Bi. Geun-hye amesema Korea kaskazini ikijaribu kutupa hata jiwe katika ardhi ya nchi yake itakiona cha moto. Hii ni katika hali ambayo, Korea Kaskazini ilitangaza siku kadhaa zilizopita kwamba imeingia katika hali ya vita na kwamba iko tayari kuzima ngebe za Marekani na Korea Kusini. Tangazo hilo limewatia tumbojoto viongozi wa Washington na Seoul ambapo hapo jana, ndege za kivita za Marekani aina ya F-22 zenye uwezo wa kukwepa rada zilifanya mazoezi katika Peninsula ya Korea. Weledi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa hatua hiyo ya Marekani ya kufanyia majaribio ndege hizo, ni onyo kwa Pyongyang kwamba itakiona cha mtemakuni ikithubuti kuishambulia Korea Kusini. Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya mambo katika Peninsula ya Korea na kuzitaka Seoul na Pyongyang kukoma mara moja kupiga ngoma za vita katika eneo hilo. Pande mbili hizo ziliwahi kupigana vita vikali kati ya mwaka 1950 – 1953 na kisha kusaini makubaliano ya usitishaji vita kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO