Tuesday, April 16, 2013

MAHAKAMA YAAMURU MUBARAK AACHIWE HURU

Mahakama moja nchini Misri imeamuru kiongozi wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, aachiwe huru kutokana na makosa ya mauaji ya waandamanaji, lakini ataendelea kubakia rumande kutokana na uchunguzi unaoendelea wa makosa ya udanganyifu. Vyombo vya habari vya Misri, vimeripoti kuwa Mahakama ya Rufaa mjini Cairo, imefikia uamuzi huo baada ya muda wa miaka miwili wa Mubarak kubakia rumande, kumalizika. Kesi ya kukata rufaa, kupinga hukumu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa dhidi ya Mubarak, ilikubaliwa kusikilizwa tena. Awali, Mubarak alihukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji. Mubarak, aliyeitawala Misri kwa miongo mitatu, aliondolewa madarakani wakati wa vuguvugu la mapinduzi mwaka 2011 na tangu Aprili 2011, anashikiliwa rumande kwa makosa ya mauaji na jaribio la kufanya mauaji ya mamia ya waandamanaji, walioandamana kwa amani kuanzia Januari 25 hadi 35, mwaka 2011. Pia anakabiliwa na mashitaka kadhaa ya ufisadi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO