Thursday, April 11, 2013

MKUTANO WA MAWAZIRI WA G8 WAFANYIKA LONDON

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, na mawaziri wengine wa mambo ya kigeni wa nchi za G8 leo wanakutana kwa siku ya pili ya mazungumzo jijini London, yanayoulenga mzozo wa Syria baada ya waasi kwa mara nyingine kuomba msaada wa silaha. Mawaziri hao walikutana jana jioni, muda mfupi baada ya viongozi wa upinzani Syria kukutana na Kerry ambapo walirudia wito wa kupewa silaha za kusaidia kupambana na majeshi ya utawala wa Syria. Mpango wa nyuklia wa Iran, mvutano unaoongezeka katika Rasi ya Korea, migogoro ya kaskazini na Magharibi mwa Afrika na mabadiliko ya tabia nchi, pia ni mada zitakazojadiliwa leo. Kerry amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, katika jitihada za kutafuta msimamo wa pamoja na mshirika huyo mkuu wa rais wa Syria, Bashar al-Assad, wa kumaliza mgogoro huo. Mkutano huo, hata hivyo umegubikwa na taarifa ya jana kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Al Nusra nchini Syria likitangaza kuwa tiifu kwa kiongozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri, jambo linaloongeza shaka ya nchi za magharibi kuhusu kuwapa waasi silaha.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO