Marekani imeionya Korea ya Kaskazini kuwa inaelekea mahali pabaya wakati nchi hiyo ikitarajiwa kufanya jaribio la kombora ambalo huenda likaanzisha tena duru mpya ya mvutano katika kanda hiyo ambayo tayari ina wasiwasi. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amesema Marekani imejiandaa kikamilifu kwa hatua yoyote ambayo Korea ya Kaskazini itachukua au uchochezi ambao huenda ikafanya. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, amewasili nchini Korea ya kusini kwa mazungumzo ikiwa ni ziara ya kwanza kuwahi kufanywa nchini humo na kiongozi wa jeshi hilo la washirika. Anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni, Yun Byung Se, na Waziri wa Ulinzi, Kim Kwan Jin, pamoja na Rais Park Geun Hye. Majeshi ya Korea ya Kusini na Marekani yako katika hali ya tahadhari huku wataalamu na maafisa wakishauri kuwa jaribio la kombora linaweza kufanywa kabla ya Aprili 15 wakati wa sherehe za siku ya kuzaliwa rais wa kwanza Kim Il-Sung. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, pia anatarajiwa kuwasili nchini humo kesho Ijumaa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO