Tuesday, April 09, 2013

NCHI ZA KIARABU ZARUDISHA NYUMA UCHUMI WA MISRI


Vita vya kiuchumi vinavyoendeshwa na nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi dhidi ya Misri vimemsababishia mgogoro mpya Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo.
Ripoti mbalimbali zinasema kuwa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait zimezidisha hitilafu zao na serikali ya Mursi kwa kuchukua uamuzi wa kuondoa vitega uchumi vyao nchini Misri. Saudi Arabia hivi karibuni iliwaweka chini ya mashinikizo viongozi wa Misri ikitaka kuondolewa nchini humo dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak pamoja na familia yake. Uhusiano mkubwa wa viongozi wa Saudia na dikteta wa zamani wa Misri umefikia kiwango ambacho Riyadh ilipendekeza kutoa kitita kikubwa cha fedha mkabala wa kufanikisha zoezi la kuachiwa huru Mubarak na familia yake. Hata hivyo serikali ya Cairo haijakubali pendekezo hilo licha ya hali isiyoridhisha ya sasa na mgogoro wa kiuchumi unaoisumbua Misri.
Wakati huo huo hatua ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Misri ya kutoa amri ya kusimamisha shughuli za wafanyabiashara 23 wakiweno matajiri kadhaa wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi imezidisha kasi ya kuondolewa vitega uchumi vya Waarabu nchini Misri. Wafanyabishara wa Kiarabu wanadai kuwa kuwekeza vitega uchumi nchini humo kwa sasa kuna hatari kubwa kwa kuzingatia hali ya kisiasa na kiusalama isiyoridhisha nchini humo. Kwa hiyo kuondolewa vitega uchumi hivyo kutakwamisha miradi 44000 nchini Misri sambamba na kuzidisha nakisi ya bajeti, ukosefu wa ajira na mdororo mkubwa wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa serikali ya Mursi imelazimika kutekeleza mpango wa kubana matumizi na kupandisha bei za baadhi ya bidhaa ili kuokoa uchumi wa nchi hiyo. Wakati huo huo kuchukuliwa hatua kama za kupandisha bei za bidhaa na ushuru mkubwa kwa baadhi ya huduma kumewakasirisha raia wa Misri. Mamia ya wananchi wa Misri hivi karibuni waliandamana katika Medani ya al Saa'a ili kulalamikia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini humo.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa matatizo hayo ya kiuchumi, mgogoro wa kisiasa na uingiliaji wa wageni yote hayo yamekuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Cairo.
Hivi karibuni Jumuiya ya al Jihad ya Misri ilimtaka Rais Muhammad Mursi ajibu matakwa halali ya wapinzani na kusafisha vyombo vya sheria kwa kufukuza masalia yote ya utawala wa Mubarak. Makundi mbalimbali ya kisiasa pia yanaonekana kukosa uvumilivu na yanataka kuondolewa nakisi na mapungufu yote yaliyobakishwa na utawala uliopita. Hii ni katika hali ambayo kutekelezwa marekebisho ya aina hiyo kunahitajia umoja, muda na utulivu kote nchini Misri.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO