Mapigano mapya yalizuka tena jana baina ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Amani Kabasha, Msemaji wa kundi la M23 ametangaza kuwa, mapigano baina ya wapiganaji hao na jeshi la serikali yanaendelea kushuhudiwa katika mji wa Goma. Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kanali Olivier Hamuli, amethibitisha habari ya kuzuka upya mapigano baina ya jeshi na waasi wa M23 lakini amekataa kutangaza idadi ya wahanga waliopoteza maisha yao katika mapigano hayo. Kanali Hamuli amesema, vitendo vya mauaji na mashambulizi yanavyofanywa na waasi wa M23 vimeshadidi tangu juma lililopita. Mapigano hayo yanahesabiwa kuwa ni ya kwanza tangu waasi wa M23 walazimike kurejea nyuma kutoka katika mji wa Goma, mwezi Disemba mwaka jana. Mapigano baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yalianza takriban mwaka mmoja uliopita na hadi sasa yamekuwa na athari mbalimbali mbaya ikiwemo ya raia wengi kulazimika kuwa wakimbizi. Waasi wa M23 walilazimika kuondoka Goma baada ya kuandamwa na jamii ya kimataifa na kupewa ahadi ya kufanyika mazungumzo baina yao na serikali. Mapigano hayo mapya yamezuka katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umekuja na mpango mpya wa kupeleka kikosi ambacho kitakuwa na uwezo wa kuingilia mapigano huko Kongo lengo likiwa ni kuzuia kuzuka tena mapigano mapya. Hii ni katika hali ambayo, wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kutumwa kwa kikosi hicho ni aina fulani ya kuchochea moto mgogoro wa nchi hiyo. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hali ya mambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imezidi kuzorota zaidi hasa baada ya Umoja wa Mataifa kubadilisha jukumu la vikosi vyake vya kusimamia amani katika nchi hiyo na kupewa uwezo wa kuingilia mapigano. Fauka ya hayo, uamuzi huo unatajwa kuwa na taathira hasi hata katika suala la kutiwa saini hati ya makubaliano baina ya serikali na waasi wa M23. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 28 Machi mwaka huu lilipasisha azimio nambari 2098 na hivyo kuvipa idhini vikosi vya Umoja wa Mataifa vya Kongo kuendesha operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi. Kwa muktadha huo vikosi vya askari wa kofia ya bluu wa Umoja wa Mataifa ambao walikuwa wakisimamia amani tu, sasa watakuwa wakishiriki katika operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya waasi. Inatarajiwa kuwa kikosi hicho kitaundwa na askari elfu tatu kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini. Kupasishwa azimio hilo kunahesabiwa kuwa chanzo cha waasi wa M23 kubadilisha msimamo wao. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, uungaji mkono wa serikali za kieneo kwa waasi hao ni chanzo cha kuzuka tena mapigano huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumatano ya kesho baada ya kutembelea Goma anatarajiwa kuelekea Rwanda na Uganda. Uganda na Rwanda zimekuwa zikituhumiwa kwamba, zinawaunga mkono waasi wa Kongo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO